Monday, 15 February 2016

Saturday, 7 February 2015

KATIBA MPYA, MGOMBEA HURU KUKUZA DEMOKRASIA TANZANIA

No comments:

NA  JACKLINE MAJURE ( WAKILI  MAHAKAMA  KUU)

Ibara ya  216.-(1)  katika rasimu inayopendekezwa  ili  iwe katiba  kama itapita  inasema kama  ifuatavyo  Bila kuathiri masharti ya Ibara ya 88 na Ibara ya 140, mtu atakuwa na haki ya kuwa mgombea huru katika uchaguzi unaosimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi.

Ni kwa maana hii  kuwa  ule utaratibu  wetu  wa kuwa  kila mgombea  ubunge au urais  au udiwani  ni lazima awe ametokana na chama chochote  cha siasa  utakuwa umekufa. Haufi  kwa maana kuwa vyama sasa  vimepigwa marufuku hapana,  isipokuwa  si lazima kupitia chama cha siasa ili mtu awe kiongozi  kwa  njia ya  kuchaguliwa.

 Mgombea huru atakuwa  ni mgombea ambaye hatokani na chama chochote cha  siasa na ataweza  kugombea  ubunge udiwani na hata  mamlaka makubwa ya urais  ataruhusiwa  kugombea. Pia ugombea huru umeainishwa kama sifa maalum kwa mtu ambaye  havutiwi  na siasa za vyama katika kugombea ubunge. Ibara  ya 140( 1 ) inasema hivi  

“Bila kuathiri masharti yaliyomo katika Ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge endapo:

(a) ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja wakati wa kugombea;


(b) anajua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kingereza; na


(c) ni mwanachama aliyependekezwa na chama cha siasa au mgombea HURU.


Baada ya kutimiza sifa  zilizoainishwa ambazo ni  kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano,  kujua kusoma  na kuandika  kati  ya  lugha  ya  Kiswahili  ama kiingereza lakini  basi  mtu asiye  na chama chochote cha siasa   anaweza  kuomba  ridhaa  ya wananchi ili awe mwakilishi wao bungeni.  Kwa mamlaka ya rais Ibara ya 88  baada ya sifa nyingine kutimia  imetoa ruksa  kwa mgombea huru  kuwania mamlaka hayo  kama ifuatavyo ; 

88.-(1) Mtu atakuwa na sifa ya kuchaguliwa kushika nafasi ya madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ikiwa:

(a) ni raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano


(f) ni mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa au mgombea   HURU.



Aidha katika yote hayo  ibara ya 143.-(1) inaibua  kitu kingine  kuhusu mgombea binafsi kama inavyonukuliwa hapa, “Mbunge atakoma kuwa Mbunge ikiwa litatokea lolote kati ya mambo yafuatayo:

(h) Mbunge aliyetokana na mgombea huru, atajiunga na chama chochote  cha siasa”


Kawaida tumezoea kusikia  diwani,mbunge au rais akiacha  chama  chake cha siasa anapoteza hata mamlaka yake. Ni kwasababu hii tumeshashuhudia mara nyingi baadhi ya viongozi wa siasa  wakikimbilia mahakamani kulinda nyadhifa zao baada ya  kutishiwa uanachama wao kwenye  vyama vyao  vya siasa.  Kwahiyo kama zamani  kuacha uanachama ilikuwa ndio upoteze mamlaka sasa   hata kuingia uanachama  nako  kutampelekea mwanasiasa kupoteza mamlaka.  Kwa ufupi tuangalie  faida na hasara   za mgombea huru  katika  ibara hizi.

FAIDA   ZA  MGOMBEA  HURU

( a ) Kwanza imepanua wigo wa demokrasia kwa  kuwashrikisha  watu wengi zaidi  katika  kuomba ridhaa ya nyadhifa  mbambnali. Wako watu wengi ambao walikuwa wakitaka  nyadhifa za siasa lakini hawapendi  siasa  za vyama. Kwa  ibara hii ni kusema kuwa hawa  nao wameingizwa katika kinyanganyiro  na hivyo sasa ushiriki utaongezeka.

( b ) Mgombea  binafsi atongeza ushindani  hasa majimboni. Wako watu ambao walikuwa na uwezo mzuri wa  kuwa  viongozi na wanakubalika  sana  kwa wananchi  lakini wanaenguliwa  katika kinyanganyiro  kutokana na hila ndani ya vyama. Kwa kuwapo mgombea  huru  itakuwa  chama kikimuengua mtu  anayekubalika  kwa wananchi  basi kijiandae kupambana naye  kwa ushindani mkubwa  katika uchaguzi.

( c )Itapelekea kupatikana  viongozi wenye uwezo  kiuongozi na si kiongozi mwenye  uwezo kimtandao  wa siasa. Mara nyingi viongozi wanaopatikana kupitia vyama vya siasa ni wale wenye  mitandao madhubuti katika vyama hivyo  na si wale wenye uwezo  kuiongozi. Hili wala sio siri  viongozi wetu wengi  wamepatikana kwa nguvu za mitandao hasa mitandao fedha  na si uwezo binafsi kiuongozi

0784482959,      0714047241




Continue Reading...

WAKULIMA, WAFUGAJI,WAVUVI NI HAKI SASA KUISHITAKI SERIKALI WASIPOTENGEWA MAENEO MAALUM, KATIBA MPYA

No comments:
NA  EMMANUEL  MARWA  ( WAKILI  MAHAKAMA  KUU).

Rasimu inayopendekezwa ili  iwe katiba inayo mambo mengi mapya.  Ni sahihi kusema mapya  kwakuwa  ni mambo ambayo hayapo katika  katiba yetu tuliyonayo  sasa. Moja ya mambo hayo  ni hili la kuingiza  au kuweka  haki za  wafugaji na wakulima, wachimbaji na wavuvi. Haya  ni  makundi muhimu sana katika jamii yetu  hasa kutokana  na ukweli  kuwa mpaka sasa  kundi  kama la wakulima  ndilo linaloonekana kubeba asilimia kubwa ya watu wote katika nchi hii.
Kwa ukweli kama huu kupata  katiba au  sheria ambamo  haki na  mustakabali wa watu kama  hawa unatajwa    si jambo la kubeza.  

( a ) MALALAMIKO   YA   MAKUNDI  YA  WAKULIMA, WAFUGAJI, WAVUVI,  WACHIMBA  MADINI.

Kwa  muda mrefu sasa  kumekuwepo  na malalamiko  kutoka kwa  makundi  hasa ya  wakulima  , wafugaji na wachimba  madini.  Malalamiko yao makubwa wamekuwa  wakiyaelekeza kwa serikali  na kubwa  zaidi wakiilalamikia  serikali kutokuwa na sera maalum ya kuwatengea  maeneo ya  kulima, malisho, kuvua  pamoja  na  maeneo  ya kuchimba madini.

Hali hii haikuwa imeishia katika malalamiko tu bali ilishapiga hatua  na  kuwa  mgogoro mkubwa  ambao sasa ulikuwa unaelekea kuwa janga la kitaifa. Na hali ilikuwa inakuwa mbaya  zaidi pale makundi haya yanapoanza  kugombea maeneo  kwa mfano  tumeshuhudia  mara kwa mara tena katika maeneo mbalimbali ya  nchi  kundi la wakulima  na kundi la wafugaji  wakigombea maeneo.

Hali ilikuwa tete  hasa pale ilipokuwa ikiripotiwa  vifo  na majeruhi kutokana  na magomvi  hayo. Tatizo kubwa ilikuwa ni kukosekana  kwa hiki ambacho  sasa kinaelezwa na rasimu hapa  chini.

( b ) WAKULIMA, WAFUGAJI, WAVUVI, WACHIMBA MADINI  KUTENGEWA MAENEO  YAO   RASMI.

Ibara  ya 46 ( 2 ) inasema kuwa  Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa kisheria kwa madhumuni ya kubainisha na kutenga maeneo ya ardhi kwa ajili ya matumizi ya  kundi la  Wakulima, wafugaji, wavuvi na wachimbaji madini. Ibara  kama hii ni ibara  muhimu  kwa mustakabali wa  uchumi na amani ya  nchi yetu.Makundi ya jamii hizi  ni makundi  ambayo yamekuwa  yakiongezeka  kwa kasi ya ajabu.

Hatari kubwa ambayo imekuwa  ikitukabili kama taifa ni kuwa  wakati makundi ya wakulima, wafugaji na wavuvi yakiongezeka  kwa haraka mno  ardhi tuliyonayo imekuwa ikibaki ileile. Hii ni kusema kuwa mahitaji ya ardhi yanaongezeka wakati ardhi haiongezeki. Kwa usemi huu  kila mtu anaweza akapima hatari ambayo kama taifa tulikuwa tunaanza kukabiliana nayo.

Ni  bomu kubwa lililokuwa  likijitega taratibu. Kutokana na hali  kuwa  hivi  ilikuwa  basi  inahitajika sera madhubuti ya kudhibiti hali hii. Na sera  ya kudhibiti hali kama hii haikupaswa kuwa  sera ya kawaida.  Ilitakiwa  kuwa sera inayotokana  na sheria kuu kama katiba. Na  hiki  ndicho  kilichofanyika.Pamoja na hayo zipo haki nyingine za makundi haya kama  tutakavyoona hapa chini.

( c ) SASA  NI LAZIMA  WAKULIMA, WAFUGAJI  KUPEWA  TAARIFA  KUHUSU  SHUGHULI   ZAO.

Ibara hiyohiyo ya 46 (b) inazidi kusema kuwa wakulima.wafugaj,wavuvi na wachimba madini watakuwa na haki ya  kupata taarifa na maarifa kwa lengo la kuboresha kilimo, ufugaji, uvuvi na uchimbaji madini.Hapo juu  tumeona haki ya makundi haya kutengewa maeneo maalum. Hapa sasa tunaona haki yao  ya kupata taarifa  ikiwa ni pamoja na maarifa.

Taarifa maana yake  ni kuwa serikali sasa inalazimika kuweka mitandao  ya kuwapasha habari wakulima, wafugaji na wachimba madini kuhusu shughuli zao. Kwa hiyo kuwapasha habari  si hiyari tena isipokuwa lazima maana ni takwa la kikatiba.

Kwa upande wa maarifa  ni kama kuwaaandalia semina, majukwaa  ya mijadala ya kielimu,kuwaunganisha  na shule za kilimo,mifugo na uvuvi, vipeperushi na vijarida na kuwaandaa kwa kila kitu kuhusu elimu. Hili nalo si la hiyari tena kwakuwa litakuwa kikatiba.

( d ) WAKULIMA, WAFUGAJI,  WACHIMBA  MADINI  NA  HAKI   YA   KUMILIKI ARDHI.

Ibara hiyohiyo ya 46 ( a ) inawapa tena  wakulima, wafugaji,wavuvi, wachimba madini haki ya kumiliki ardhi kwa  kusema kuwa (a) wakulima, wafugaji,wavuvi, wachimba madini watakuwa na haki ya kumiliki, kutumia na kuendeleza ardhi kwa ajili ya shughuli zao;    
Kama Watanzania wengine  haki  ya kutumia  na kumiliki ardhi  walikuwa nayo hata kabla ya rasimu hii.
Lakini sasa kuiweka katika Katiba  na huku ikiwarejea wao peke yao  ni jambo la mafanikio  na  linaloonesha ni kwa namna  gani  ipo ari  ya kushughulikia matatizo yao.  Pia inaonesha ni kwa kiasi gani  makundi haya sasa yanatambulika rasmi  na haki zao zinatofautishwa  na haki za makundi mengine.

( e ) UMUHIMU  AU  FAIDA  KATIKA  IBARA  HIZI  JUU.

Kuna kitu kikubwa kimoja ambacho kinajitokeza  na kuwa kama faida kubwa ya ibara  nilizoeleza hapa juu. Kutokana na ibara kuwa katika mtindo huo tuliouona hapo juu  sasa ieleweke wazi kuwa  makundi  yote yaliyotajwa katika ibara  hizi  yamepata  ruhusa  ya  kuifungulia  mashtaka serikali  iwapo lolote katika  yaliyoorodheshwa kama haki  zao  hayakutekelezwa.

Hii ina maana  baada ya kupita kwa rasimu na  kuwa katiba wakulima, wavuvi, wachimba madini wasipotengewa maeneo maalum kwa ajili ya shughuli zao  basi  wanaweza kuishtaki serikali  kwa maombi maalum( petition)  na wakapata haki  hizo  ikiwemo fidia.  Kwa hiyo sasa ni kusema kwamba suala la serikali kutenga maeneo maalum kwa ajili  ya  makundi  haya  sasa ni la  lazima.
 0784482959, 0714047241



Continue Reading...

KATIBA MPYA, KIGEZO CHA SHAHADA KWA MGOMBEA URAIS SASA KUTUPATIA RAIS BORA .

No comments:


NA  BASHIR  YAKUB (MWANASHERIA  MWANDAMIZI)

Ni siku muhimu tena katika uchambuzi wa Ibara mbalimbali katika rasimu inayopendekezwa ili  ikipita iwe  katiba. Upo umuhimu mkubwa sana kwa Watanzania kujua kilichomo ndani ya  rasimu hii kwakuwa  leo hii inaitwa rasimu lakini kesho itaitwa sheria  na kila mtu anayejua kilichomo na asiyejua wote watalazimika kuwajibika kwake bila kukiuka .

Kwa msingi huu elimu na hamasa zaidi inahitajika ili kumfanya kila  mtu aone hili linamhusu kabla ya kuanza kulalamika kwa kuonewa itakapoanza kutekelezwa kwa lazima. Katika mwendelezo wa uchambuzi wa Ibara zilizomo katika rasimu  leo tujikite katika Sura ya  Nane Sehemu ya Kwanza ( b ) Ibara ya 85 ( 1 ) ( e )  ambayo inanukuliwa hivi

“Mtu atakuwa na sifa ya kuchaguliwa kushika  nafasi ya madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ikiwa anayo shahada ya chuo cha elimu ya juu kinachotambuliwa kwa
mujibu wa sheria, au awe na ujuzi na uzoefu wa uongozi katika
ngazi ya taifa utakaomwezesha kumudu madaraka ya Rais”

Ibara ya namna hii  ni mara ya kwanza kabisa katika historia ya nchi yetu  kuingia katika katiba. Pamoja na mabadiliko mengi yaliyowahi kufanyika kwenye katiba kigezo hiki hakikuwahi kuingizwa.

Siwezi kusema  waliopendekeza  ibara hii kuwemo walilenga nini lakini  kwa akili ya kawaida  kabisa utaona kuwa wamezingatia zaidi mabadiliko makubwa ya kidunia. Hapo awali  sifa ya kuwa mgombea urais ilikuwa uwezo wa kujua na kusoma na kuandika. Aliyejua kusoma na kuandika  na sifa nyingine  ilimtosha kuizuru tume tayari kwa kuchukua fomu ya nafasi ya rais.

Leo rasimu ikipita  ina maana hata  mwenye stashahada(diploma) haruhusiwi kuusogolea urais.
Aidha ukiisoma vizuri ibara utaona kuwa hata stashahada ya juu ( Advanced diploma) ambayo  kwa mwenendo wetu wa elimu imekuwa ikichukuliwa kuwa na hadhi sawa  na shahada(degree) imekataliwa katika kuukwaa urais.

Kitu kingine ambacho kimejitokeza katika ibara hiyo ni  pale inapoainishwa sifa nyingine ambayo  ni ujuzi na uzoefu  wa uongozi katika ngazi ya taifa  utakaomwezesha kumudu madaraka ya rais.  Ibara imekaa hivi,  kwanza awe na shahada  ya kwanza  kutoka chuo kinachotambulika  au awe na uzoefu na ujuzi katika uongozi ngazi ya taifa wa kumwezesha kumudu madaraka ya rais.

Nimekariri hilo neno “au” hapo juu kwakuwa lina maana kubwa katika  ibara hii. Maana  ya neno au ni kuwa  anayeutaka urais awe na kimoja kati ya  elimu ya shahada au  uzoefu.  Hii maana yake ni kuwa inawezekana ukawa hata  na elimu ya darasa la saba  lakini ikiwa unao uzoefu  katika uongozi wa taifa basi umepata sifa kikatiba  ya kugombea.

 Ingekuwa  imesema awe na shahada  pamoja na uzoefu basi  ingekuwa maana yake vinatakiwa vyote viwili lakini kumbe  hata kimoja tu elimu au uzoefu  inakuwa tayari ni sifa  kwa mujibu wa ibara hii. Ufafanuzi wetu hapa huwa ni ufafanuzi wenye uwiano(balanced description). Huwa inaelezwa ibara  kama tulivyoona hapo juu halafu zinaelezwa faida zake na hasara zake ili iwe nafasi kwa msomaji mwenyewe kwa kutumia akili kuona lipi jema kwa mustakabali wa leo na kesho katika taifa na lipi si jema.Hivyo basi hapa chini zinaelezwa faida na hasara za Ibara hii.

FAIDA  AU  UZURI  WA IBARA  HII.

( a ) Kwanza kabisa kwa kuweka kigezo cha elimu  ya kiwango cha juu kama shahada  ibara hii  imezingatia sana hatua kubwa ambayo dunia imepiga. Ukweli ni kuwa uendeshaji wa nchi wa sasa  ni uendeshaji unaohitaji uelewa mkubwa unaotokana  pamoja na mambo mengine na kiwango kikubwa cha elimu  kama shahada.  

Yapo mambo makubwa ya  kitaalam yanahitaji ukokotozi na uelewa wa hali ya juu kwa mfano  mambo ya miamala ya kodi, sheria za kimataifa, mikataba mikubwa, upangaji wa sera  makini, uwezo wa kutafiti  na kuendana na mabadiliko makubwa ya kiteknolojia n.k.

Hayo yote yanahitaji shule kubwa   kwa hili wala tusiongee sana.  Ni kweli rais anakuwa na wasaidizi wake ambao kimsingi ndio wataalam haswa. Lakini hilo haliondoa ulazima wa yeye kutakiwa kujua mambo hayo pia. Hii ni kwakuwa pamoja na mambo kufanywa na wasaidizi mwisho wa siku lazima naye apitie na atoe ushauri, amri au maagizo kuhusiana nayo. Atawezaje kutoa maagizo kwenye mikataba mikubwa ya kiamataifa au jambo kubwa linalohusu sera  za nchi bila kuwa na elimu kubwa.

Atashauri nini kama hajui. Si atakuwa wa kudanganywa na watendaji na mwisho wa siku taifa linaangamia. Huo ni ukweli mtupu  na hakuna namna ya kuusema isipokuwa hivihivi ulivyosemwa.  Kwa ufupi twaweza kusema kuwa kwa ibara hii tutampata rais mweledi( professionalism)  na huu ndo utakuwa uzuri wa kwanza wa ibara hii.

( b )Faida au uzuri mwingine wa ibara hii ni kuwa  kwa kusema kuwa mtu awe na shahada  au ujuzi na uzoefu katika uongozi ibara imejitahidi kuwaingiza watu  wengine ambao hawatakuwa na shahada lakini wamekuwa katika uongozi kwa ngazi ya taifa kwa muda mrefu, wamekuwa waadilifu na wanao ujuzi wa kutosha  wa kuwawezesha kushika kiti cha rais.

Ni ukweli kuwa kuwa ndani ya serikali wamo watu wengi ambao hawana hizi shahada lakini wamekuwa katika uongozi wa taifa kwa muda mrefu  na wanao ujuzi wa kuongoza pengine kuliko hata hao wenye shahada zao. Tunao wanasiasa wengi wakongwe  ambao wengi wao kutokana na kusoma zamani au  vinginevyo  hawana  shahada lakini ni wazuri sana  katika uongozi. Wapo wengine waliwahi kuwa mawaziri huko nyuma, makatibu wakuu, wabunge na nyadhifa nyingine nyingi. Hawa nao wamepewa nafasi na ibara hii kwa sifa yao ya ujuzi na uzoefu.

0784482959
0714047241




Continue Reading...

TUJIHADHARI NA MATUMIZI YA DEMOKRASIA, KATIBA MPYA

No comments:

NA  EMMANUEL  NDANU (WAKILI  MAHAKAMA  KUU)

Sura ya pili, sehemu ya pili  ibara ya 12( 1 ) ya rasimu inayopendekezwa kuwa katiba  inasema kuwa
“Lengo la Katiba hii kisiasa ni kudumisha demokrasia”.
Rasimu inayasema haya ikiwa katika harakati za kuelezea malengo ya taifa ya kisiasa.Kimsingi  katika rasimu yako malengo ya taifa ya kijamii( social vision), malengo ya taifa ya kiutamaduni( cultural vision), malengo ya taifa ya kiuchumi( economic vision) na malengo ya taifa  kisiasa( political vision) ambayo  ndio  tunayaangalia sasa.

Ukisikia malengo ya taifa kisiasa au kijamii maana yake ni mwelekeo  wa taifa  kisiasa au kijamii. Mwelekeo maana yake ni kuwa  kila kitakachokuwa kinafanyika nchini lazima kiwe kinafanana na kile kilichosemwa  katika katiba. Taasisi zote za  dola na za kiraia   lazima zihakikishe shughuli zake zote zinafanana na lengo la kisiasa katika katiba. Na kwakuwa lengo la kisiasa ni demokrasia basi  kila taasisi ya kidola au binafsi lazima ihakikishe  shughuli zake zinafanana  na demokrasia.

Hii maana yake ni kuwa  demokrasia itakuwa ndio kioo. Taasisi au mtu binafsi atakuwa anatakiwa kujitazama  na kuona kama anafanana na  demokrasia iliyosemwa katika katiba ambapo akiona anafanana  basi hiyo shughuli anayoifanya ni halali  kwakuwa ina baraka za katiba na akiona haifanani basi shughuli hiyo ni haramu na yuko katika hatari ya kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kukiuka katiba.

Ni sawa na kusema  kuwa demokrasia kiwe ndio kiigizo chetu, iwe ndio mfano wetu.Hiyo ndio maana ya demokrasia kuwa lengo la taifa kisiasa. Kwa maneno kama haya utaona ni kwa namna gani demokrasia imetukuzwa  na kupewa hashima ya pekee kiasi cha kupendekezwa kuwa kiigizo kwa Watanzania zaidi ya milioni 45.

 Hii demokrasia nini mpaka ipate heshima kubwa kiasi  cha  kuwa lengo kuu,kiigizo kikuu, mwelekeo mkuu, na mfano mkuu  wa watu zaidi ya milioni 45 kitaifa.     

DEMOKRASIA   NININI.

Ziko tafsiri nyingi na maarufu za demokrasia ambazo wengi wetu  tunazijua. Sitaeleza tafsiri yoyote katika hizo isipokuwa nitaeleza wazo la jumla kuhusu hiki kitu kinachoitwa demokrasia ambacho  katiba yetu mpya  imetuelekeza kukisujudia.

Ukitaka kumweleza  mtu wa kawaida kabisa maana  ya demokrasia mwambie hivi, demokrasia ni haya maisha unayoyaona sasa,watu wanavaa wanavyotaka, watu wanatembea kulala na kula wanavyotaka, mtu anaamua awanie uongozi au hapana, mtu anaamua  nani awe kiongozi wake na nani asiwe, mtu anaoa au kuolewa na anayemtaka, mtu  anamkosoa anayemtaka awe kiongozi wake mkuu  au mdogo, mtu anazungumza anavyotaka , mtu anaruhusiwa kuishi popote na bila kubughudhiwa, yaani kwa  ufupi kila uhuru wa kutenda jambo unaouona hiyo ndio demokrasia.Mtu atakuelewa vyema.

DEMOKRASIA  NDIO  UBEPARI

Matendo ya kufanya mambo kwa uhuru yameanza mamilioni ya miaka iliyopita isipokuwa hayakuwa yakiitwa demokrasia. Walioanzisha demokrasia walichukua baadhi ya  matendo huru wakayaingiza katika huo mfumo wao wakayaita demokrasia.

 Lakini matendo kama uhuru wa kuongea(maoni), kutembea , kuvaa n.k yalikuwapo kabla ya kitu kiitwacho demokrasia na umri wa matendo haya waweza kuwa sawa na umri wa mwanadamu duniani.Aidha demokrasia hii tuliyonayo leo imeanza karne ya 15  kipindi cha hatua ya kwanza ya ubepari( mechantalism) na imekua mpaka hatua ya sasa ya ubepari  ambayo huitwa ubepari uliokomaa(monopoly capitalism).

Kimsingi demokrasia ndio sera kuu ya ubepari na neno demokrasia limeanzishwa na mabepari.  Kwa maana hiyo tunapoamrishwa na katiba kuwa demokrasia iwe ndio  kiigizo, chetu, na mfano wetu tunaambiwa kuwa kiigizo, na mfano wetu uwe ubepari.Ubepari(Capitalism) ndio unaomiliki kitu kiitwacho demokrasia hili wala halina shaka. Kwa ibara hii maana yake ni kuwa mwelekeo wa nchi hii ni ubepari na nchi hii sasa ni ya kibepari rasmi.

MATATIZO  YA  KUFUATA  UBEPARI.

( a ) Ielewewke kwamba ubepari ni mali ya watu na bila shaka walioanzisha na kumiliki mali hiyo wanayo malengo yao. Miaka ya nyuma kiongozi wa ubepari alikuwa Wingereza na sasa kiongozi wa ubepari ni Marekani. Wakati Wingereza akiongoza ubepari alitumia nafasi hiyo  hasa kwa mgongo wa demokrasia  kuingia Afrika na kuitawala Afrika akishirikiana na wenzake wa ulaya.

Walijifanya wamekuja  na mfumo mpya wa uongozi ambao ungeweza kumaliza matatizo  na shida za watu huku wakijua na kuamini kuwa  mfumo huo wenyeji wasingeweza kumudu misingi yake kutokana na elimu na weledi mdogo na hivyo kujikuta wameangukia mikononi mwa wageni.Kwa ufupi tuliweza kutawaliwa kwa urahisi kutokana na kuzidiwa na mbinu za hiki kinachoitwa demokrasia.  

( b ) Leo Amerika ameweza kuwa na amri juu ya dunia kupitia hiki kitu kinachoitwa demokrasia. Mila na tamaduni za asili ambazo zimezaa maadili mema na mwenendo mwema katika jamii zetu kwa muda mrefu zimekufa  na zimeuliwa na hiki kiumbe demokrasia.Tunashuhudia mavazi ya hovyo,vitendo  vya ukahaba, ushoga, heshima kutoweka kwa mkubwa na mdogo, usagaji, na ghasia nyingine nyingi kwa mgongo wa huyu demokrasia.

( c ) Wameandaa vitu wakaviita misingi mikuu ya demokrasia huku wakiamini kuwa hakuna yeyote atakayeweza kufaidika   na vitu hivyo isipokuwa wao. Mfano, moja ya msingi wa demokrasia ni kuwa na uhuru katika uchumi au uchumi huria. Katika uchumi huru ndimo penye uwekezaji  kimataifa.

Ndani ya uwekezaji wa kimataifa ndimo  ilimo fursa ya wao kuja kuogelea katika rasilimali zetu. Walijua uhuru  katika uwekezaji wa kimataifa hakuna mwafrika atayekuwa na uwezo wa kuwekeza kitu cha maana kwao. Isipokuwa wao ndio wataokuja kuvinjari ndani ya migodi yetu,maziwa yetu, bahari, mafuta, gesi, na kila kitu.Demokrasia ni mali ya watu  na wenye nayo wanayo malengo yao.

Tunatoa uhauri kuwa pamoja  na maono  mazuri ya  katibas  mpya katika kukuza  na kuimarisha  demokrasia  tunapenda  kusema  kama alivyosema  aliyekuwa rais  wa Libya  marehemu Kanali Muammar Gaddafi  kuwa demokrasia  nzuri  ni ile isiyoharibu mila desturi za wenyeji  pia  ni ile isiyotumka  kuingiza fikra za kinyonyaji.

0784482959
0714047241

                                          
Continue Reading...

KINGA DHIDI YA MASHTAKA YA RAIS KUMFANYA RAIS AJAYE KUJIAMINI KUSHUGHULIKIA UFISADI.

No comments:

NA  JACKLINE  MAJURE  (WAKILI  MAHAKAMA   KUU)

Ibara ya 93 katika rasimu inayopendekezwa ili iwe katiba  inasema hivi 93.-(1)” Wakati Rais akiwa madarakani, hatashtakiwa wala mtu yeyote
hataendesha mashtaka ya aina yoyote dhidi yake mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai”.

Ni aina ya ibara ambayo inatoa kinga kwa mtu atakayekuwa ameshika madaraka  ya rais kutoshitakiwa. Katika ibara hii kuna  mambo matatu ya kuzingatia, Kwanza kabisa ibara hii inazungumzia  wakati rais anapokuwa madarakani yaani wakati  yuko ikulu ndo asifunguliwe  mashtaka, lakini pili mashtaka yenyewe ambayo hapaswi kufunguliwa ni yale  Mashtaka ya kijinai tu ambayo ni kama kuua, kubaka, kulawiti,kupiga, kuiba, rushwa, uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya ofisi n.k. Tatu sehemu anapozuiwa kushtakiwa ni mahakamani  wala si bungeni.

Kwa kawaida viongozi wakuu hasa marais wakati mwingine hushtakiwa mahakamani au bungeni lakini kwa hapa  imezuiwa kumshtaki makahamani wala si bungeni.Kwahiyo ibara hii ndogo ya ( 1 ) imeundwa na mambo hayo matatu.

Aidha Ibara hiyohiyo Ibara ndogo ya (2) inasema hivi  “Wakati Rais ameshika madaraka kwa mujibu wa Katiba hii,haitaruhusiwa kufungua mahakamani shauri la madai kuhusu jambo lolote alilolitenda au alilokosa kulitenda yeye binafsi kama Rais ama kabla au baada ya kushika madaraka ya Rais, ila tu kama angalau siku thelathini kabla ya shauri  kufunguliwa mahakamani, Rais atapewa au ametumiwa taarifa ya madai kwa  maandishi kwa kufuata utaratibu utakaowekwa kwa mujibu wa sheria, na taarifa  hiyo ikiwa inatoa maelezo kuhusu chanzo cha shauri hilo, kiini cha madai  yenyewe, jina lake na anwani ya mahali anapoishi huyo mdai na jambo hasa   analodai”

 Ibara hii inatoa nafasi kwa rais aliye madarakani kushtakiwa kwa makosa ya madai. Ile ibara ya kwanza ya juu inakataza kumshtraki kwa makosa ya jinai wakati akiwa madarakani. Hii sasa inaruhusu kushtakiwa hata akiwa madarakani lakini kwa makosa ya madai tu. Makosa ya madai ni kama kugombea mashamba,viwanja au nyumba, kukopeshana vitu vya thamani kama fedha na kushindwa kulipa, kudai fidia baada ya kutukanwa au kudhalilishwa,kuvunja mkataba kama mikataba ya mauziano ya vitu kama magari n.k. Hayo ndio makosa  ya madai ambayo rais hata akiwa madarakani waweza kumshtaki nayo.

Aidha jambo jingine la tofauti limejitokeza  katka ibara hiyohiyo  ya 93 ibara ndogo ya (3) ambayo inasema hivi “ Isipokuwa kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na kuondolewa madarakani na Bunge, haitakuwa halali kwa mtu kumshtaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au la madai dhidi ya mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo
alilofanya wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya Rais”.

Kwanza tuliona hairuhisiwi kumshtaki rais kwa kosa lolote la jinai pale anapokua madarakani, pili tumeona inaruhusiwa kumshtaki rais kwa kosa la madai hata akiwa madarakani na sasa tunaona kuwa itakapotokea bunge limemwondoa rais madarakani  basi hakuna ruhusa mtu  au chombo chochote kumshtaki rais kwa kosa lolote liwe la jinai au la madai alilofanya akiwa madarakani.

 Sura ya jumla ya ibara hizi zote kwa pamoja ni kuwa kwanza rais hashtakiwi kwa kosa lolote la jinai  iwe pale anapokuwa madarakani au hata baada ya kutoka. Makosa yote ya jinai aliyoyafanya wakati akiwa ikulu hayaguswi kabisa. Pili ni kuwa  anayetaka kumshtaki rais kwa kosa la madai amshtaki akiwa bado yuko madarakani lakini akishatoka basi huwezi tena kumshtaki hasa kama ametoka kwa kuondolewa na bunge. Tuangalie faida au uzuri wa ibara hizi na mapungufu au hasara zake.

FAIDA AU UZURI WA IBARA HIZI

( a ) Kwanza  unapomwekea kinga rais hasa anapokuwa madarakani ambao ndio wakati wa kutekeleza majukumu yake unakuwa umempa  uhuru na umemwondolea woga katika kuamua na kutoa maamuzi magumnu  katika  utekelezaji wa sera.

Rais anafanya mambo bila woga wala bila kuhofia lolote jambo ambalo likitumiwa vyema laweza kutoa fursa kwa kushughulikia mambo sugu yaliyoshindakana kama ufisadi hasa katika kuwashughulikia wale watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha au kimamlaka ambao hufanya matendo maovu kwa kujiamini kutokana na kujijenga katika mitandao ya siasa ambayo wakati mwingine hutishia hata mamlaka ya rais.

( b ) Pili unapoweka ugumu katika kumshtaki rais akiwa madarakani  hakika unakuwa unajenga msingi wa amani na utulivu. Kurahisisha kumshtaki rais  kama raia wa kawaida kunaweza kupelekea mashauri ya mara kwa mara dhidi yake kitu ambacho kinaweza kuliyumbisha taifa kutokana na unyeti na ukubwa wa nafasi yenyewe.

0784482959 , 0714047241



Continue Reading...

KATIBA MPYA KUMALIZA USHINDI WA UBABAISHAJI UCHAGUZI MKUU

No comments:



NA   EMMANUEL   NDANU  (WAKILI  MAHAKAMA  KUU)

Katika uchambuzi wa leo wa rasimu inayopendekezwa ili iwe katiba  tumeona ni vyema  kuifanyia mapitio sura ya 8 ya rasimu hii  ambayo kwa ujumla inazungumzia  pamoja na mambo mengine uchaguzi wa rais. Yako mambo mengi katika sura hii kumhusu rais au nafasi ya rais  lakini hayatazungumzwa yote isipokuwa itaguswa Ibara ya 86 ( 6 )   ambayo inazungumza hivi

  “ Mgombea wa nafasi ya madaraka ya Rais atatangazwa kuwa
amechaguliwa kuwa Rais iwapo atapata kura zaidi ya asilimia hamsini ya
kura zote halali zilizopigwa kwa nafasi ya madaraka ya Rais.”
Kwa  kipindi cha takribani miaka kumi na tano iliyopita hili kwetu halikuwako. Rais alikuwa  akipata ushindi hata kwa  kumzidi mwenzake kura moja. Ibara hii mpya katika rasimu  inaleta mfumo mpya wa kumpata rais. Ukifanya tathmini duniani utaona kuwa  asilimia kubwa ya mataifa ambayo hujinasibisha na mfumo wa demokrasia  hutumia mfumo huu  wa asilimia hamsini katika chaguzi zao.

Kwa walio wengi hapa kwetu hasa vijana hususan miaka thelathini kushuka wanaweza kuona kitu hiki kama kigeni sana katika  nchi yetu. Ukweli ni kuwa  utaratibu huu wa kumpata  rais kwa mtindo wa asilimia hamsini si mgeni. Itakumbukwa kuwa  Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977  ilikuwa na ibara ya namna hii  na chaguzi za kipindi hicho zilifanyika katika utaratibu wa  aliyezidi asilimia hamsini ndio mshindi.

Ni mabadiliko ya 13 ya Katiba ya mwaka 2000 ndiyo yaliyoondoa utaratibu huu na kuweka utaratibu  huu tulionao sasa  ambapo mtu anaweza kutangazwa kuwa rais  hata kwa kumzidi mwenzake kura moja. Hii ni kusema kuwa mtindo huu sasa unakufa tunaanza mtindo wa asilimia ambao ndio unaotumika kwa wingi hivi sasa duniani. Wapo wanaoona  mtindo tuliokuwa nao ni mzuri na wapo wanaoona mtindo mpya wa asilimia ni ndio mzuri zaidi. Inategemea na mtazamo hasa kimaslahi.

Kihistoria chimbuko la  utaratibu wa wingi wa kura kama tulionao na wingi wa kura kwa asilimia ilikuwa ni katika jitihada za wanazuoni katika kutafsiri maana ya neno KURA ZA WENGI (Majority Vote). Katika  harakati hizo baadhi ya wanazuoni wakaja na mawazo kuwa kura za wengi  ni ile idadi kubwa zaidi kuliko  nyingine  ikiwa na maana  hata  kumzidi mtu kura moja  tayari yule aliyemzidi mwenzake kura moja anahesabika kuwa  ndiye aliyependwa na wengi zaidi kwakuwa amemzidi mwenzake kura moja.

Wanazuoni wengine  wakakata wazo hili nao wakaja na wazo kuwa  wingi hauwezi kuhesabiwa hata kwa kuzidiana kura moja isipokuwa maana ya wingi wa kura  iwe ni wingi wa asilimia. Wakimaanisha kuwa  ikiwa wtakaopiga kura ni alfu moja  basi atakayepata zaidi ya  nusu ya hizo ambazo ni zaidi ya mia tano huyo ndiye atakayekuwa mshindi.Lakini ikiwa  mmoja amepata kura mia nne hamsini  na mwingine amepata miatatu kati ya alfu moja zilizopigwa basi  hata huyu wa 450 hatahesabiwa kuwa ameshinda.

Yote ni mawazo tu  ya wanazuoni ambayo ndio chimbuko la Ibara hii. Mitazamo yote yaweza kuwa sahihi au hapana au mmoja waweza kuwa sahihi zaidi kuliko mwingine. Zaidi ya hayo sisi pia  tuangalie faida na hasara za ibara iliyokaa katika mtindo huo.

FAIDA  AU   UZURI  WA   IBARA  HII.

( a ) Uzuri wa kwanza wa kuhesabu ushindi kwa mtindo wa zaidi ya asilimia hamsini ni kuwa  taswira halisi ya  mshindi kuwa ndio chaguo la wengi inajitokeza. Chaguo la wengi linakuwa linakuwa  chaguo la wengi kweli. Hii ni kwakuwa  mfumo huu katika kuhesabu mshindi unazingatia idadi ya waliopiga kura na aliyevuka nusu ya kura hizo.

 Kwa mfano waliopiga kura ni laki moja  hii ina maana ili mtu awe mshindi inabidi apate zaidi  ya elfu hamsini.Kimahesabu wingi wa watu laki moja ni kweli kabisa unahesabiwa kuanzia zaidi ya nusu yake ambao ni  elfu hamsini. Hivyo anayepata zaidi ya watu hao huyo kweli ndiye aliyependwa zaidi kwakuwa amependwa na zaidi ya nusu.

Wakati ingekuwa katika mfumo ule tunaotumia sasa ambao si wa asilimia hamsini  kama wapiga kura wangekuwa  laki moja  mgombea mmoja akapata  kura mia tano na mwingine akapata mia tano na mbili(502) na nyingine  zikaenda kwa wagombea wengine huyu wa mia tano na mbili angetangazwa mshindi bila kujali zaidi ya kura elfu tisini na tano(95000)  zilizomkataa. Kwa hiyo utaona kuwa mtindo wa asilimia  unajenga na kuleta taswira ya kweli katika kanuni ya wingi wa kura (majority vote) katika kumpata mshindi.

( b ) Faida nyingine ya mshindi kwa wingi wa asilimia ni kuwa  inaonesha kwa dhati  kiwango cha kukubalika kwa mshindi. Mfano mfumo tulionao sasa rais anaweza kuwa rais hata kwa kumzidi mwenzake kura moja tu.

Kwa hali ya kawaida  ukimshinda mtu kwa kura moja picha inayokuja ni kuwa pamoja na ushindi wa mgombea  wako wengi hawamkubali. Ina maana katika jamii iliyopiga kura mshindi na mpinzani wake wanalingana katika kupendwa isipokuwa  tofauti yao ni mtu mmoja tu ambaye pengine naye amepatikana kwa kuwa mshindi ana familia kubwa zaidi ya mshindwa.

Kimsingi hata  mshindi wa kwanza na wa pili wakitofautiana kura tano au hata kumi bado  utaona kuwa hata yule aliyemzidi mwenzake hakubaliki sana. Lakini kwa mtindo wa asilimia  hakuwezi kuwapo na tofauti ya kura moja , mbili, kumi ishirini, thelathini na pengine hata mia. Utofauti wa kura huwa ni mkubwa  kiasi cha kujenga taswira iliyo wazi kuwa mshindi anakubalika kwa  watu wengi zaidi kuliko  mwenzake.

0784482959
0714047241


                                                  
Continue Reading...