Ni siku muhimu tena katika
uchambuzi wa Ibara mbalimbali katika rasimu inayopendekezwa ili ikipita iwe
katiba. Upo umuhimu mkubwa sana kwa Watanzania kujua kilichomo ndani
ya rasimu hii kwakuwa leo hii inaitwa rasimu lakini kesho itaitwa
sheria na kila mtu anayejua kilichomo na
asiyejua wote watalazimika kuwajibika kwake bila kukiuka .
Kwa msingi huu elimu na
hamasa zaidi inahitajika ili kumfanya kila
mtu aone hili linamhusu kabla ya kuanza kulalamika kwa kuonewa
itakapoanza kutekelezwa kwa lazima. Katika mwendelezo wa uchambuzi wa Ibara
zilizomo katika rasimu leo tujikite
katika Sura ya Nane Sehemu ya Kwanza (
b ) Ibara ya 85 ( 1 ) ( e ) ambayo inanukuliwa hivi
“Mtu
atakuwa na sifa ya kuchaguliwa kushika nafasi
ya madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ikiwa anayo shahada ya chuo cha
elimu ya juu kinachotambuliwa kwa
mujibu
wa sheria, au awe na ujuzi na uzoefu wa uongozi katika
ngazi
ya taifa utakaomwezesha kumudu madaraka ya Rais”
Ibara
ya namna hii ni mara ya kwanza kabisa
katika historia ya nchi yetu kuingia katika
katiba. Pamoja na mabadiliko mengi yaliyowahi kufanyika kwenye katiba kigezo hiki
hakikuwahi kuingizwa.
Siwezi
kusema waliopendekeza ibara hii kuwemo walilenga nini lakini kwa akili ya kawaida kabisa utaona kuwa wamezingatia zaidi mabadiliko
makubwa ya kidunia. Hapo awali sifa ya
kuwa mgombea urais ilikuwa uwezo wa kujua na kusoma na kuandika. Aliyejua
kusoma na kuandika na sifa nyingine ilimtosha kuizuru tume tayari kwa kuchukua
fomu ya nafasi ya rais.
Leo
rasimu ikipita ina maana hata mwenye stashahada(diploma) haruhusiwi
kuusogolea urais.
Aidha
ukiisoma vizuri ibara utaona kuwa hata stashahada ya juu ( Advanced diploma)
ambayo kwa mwenendo wetu wa elimu
imekuwa ikichukuliwa kuwa na hadhi sawa
na shahada(degree) imekataliwa katika kuukwaa urais.
Kitu
kingine ambacho kimejitokeza katika ibara hiyo ni pale inapoainishwa sifa nyingine ambayo ni ujuzi na uzoefu wa uongozi katika ngazi ya taifa utakaomwezesha kumudu madaraka ya rais. Ibara imekaa hivi, kwanza awe na shahada ya kwanza kutoka chuo kinachotambulika au
awe na uzoefu na ujuzi katika uongozi ngazi ya taifa wa kumwezesha kumudu
madaraka ya rais.
Nimekariri
hilo neno “au” hapo juu kwakuwa lina maana kubwa katika ibara hii. Maana ya neno au ni kuwa anayeutaka urais awe na kimoja kati ya elimu ya shahada au uzoefu.
Hii maana yake ni kuwa inawezekana ukawa hata na elimu ya darasa la saba lakini ikiwa unao uzoefu katika uongozi wa taifa basi umepata sifa
kikatiba ya kugombea.
Ingekuwa
imesema awe na shahada pamoja na
uzoefu basi ingekuwa maana yake
vinatakiwa vyote viwili lakini kumbe
hata kimoja tu elimu au uzoefu
inakuwa tayari ni sifa kwa mujibu
wa ibara hii. Ufafanuzi wetu hapa huwa ni ufafanuzi wenye uwiano(balanced
description). Huwa inaelezwa ibara kama
tulivyoona hapo juu halafu zinaelezwa faida zake na hasara zake ili iwe nafasi
kwa msomaji mwenyewe kwa kutumia akili kuona lipi jema kwa mustakabali wa leo
na kesho katika taifa na lipi si jema.Hivyo basi hapa chini zinaelezwa faida na
hasara za Ibara hii.
FAIDA
AU UZURI WA IBARA
HII.
( a ) Kwanza kabisa kwa kuweka kigezo cha elimu ya kiwango cha juu kama shahada ibara hii
imezingatia sana hatua kubwa ambayo dunia imepiga. Ukweli ni kuwa
uendeshaji wa nchi wa sasa ni uendeshaji
unaohitaji uelewa mkubwa unaotokana
pamoja na mambo mengine na kiwango kikubwa cha elimu kama shahada.
Yapo
mambo makubwa ya kitaalam yanahitaji
ukokotozi na uelewa wa hali ya juu kwa mfano
mambo ya miamala ya kodi, sheria za kimataifa, mikataba mikubwa,
upangaji wa sera makini, uwezo wa
kutafiti na kuendana na mabadiliko
makubwa ya kiteknolojia n.k.
Hayo
yote yanahitaji shule kubwa kwa hili wala tusiongee sana. Ni kweli rais anakuwa na wasaidizi wake ambao
kimsingi ndio wataalam haswa. Lakini hilo haliondoa ulazima wa yeye kutakiwa
kujua mambo hayo pia. Hii ni kwakuwa pamoja na mambo kufanywa na wasaidizi
mwisho wa siku lazima naye apitie na atoe ushauri, amri au maagizo kuhusiana
nayo. Atawezaje kutoa maagizo kwenye mikataba mikubwa ya kiamataifa au jambo
kubwa linalohusu sera za nchi bila kuwa na
elimu kubwa.
Atashauri
nini kama hajui. Si atakuwa wa kudanganywa na watendaji na mwisho wa siku taifa
linaangamia. Huo ni ukweli mtupu na
hakuna namna ya kuusema isipokuwa hivihivi ulivyosemwa. Kwa ufupi twaweza kusema kuwa kwa ibara hii
tutampata rais mweledi( professionalism)
na huu ndo utakuwa uzuri wa kwanza wa ibara hii.
( b )Faida au uzuri mwingine wa ibara hii ni kuwa kwa kusema kuwa mtu awe na shahada au ujuzi na uzoefu katika uongozi ibara
imejitahidi kuwaingiza watu wengine
ambao hawatakuwa na shahada lakini wamekuwa katika uongozi kwa ngazi ya taifa kwa
muda mrefu, wamekuwa waadilifu na wanao ujuzi wa kutosha wa kuwawezesha kushika kiti cha rais.
Ni
ukweli kuwa kuwa ndani ya serikali wamo watu wengi ambao hawana hizi shahada
lakini wamekuwa katika uongozi wa taifa kwa muda mrefu na wanao ujuzi wa kuongoza pengine kuliko
hata hao wenye shahada zao. Tunao wanasiasa wengi wakongwe ambao wengi wao kutokana na kusoma zamani
au vinginevyo hawana
shahada lakini ni wazuri sana katika
uongozi. Wapo wengine waliwahi kuwa mawaziri huko nyuma, makatibu wakuu,
wabunge na nyadhifa nyingine nyingi. Hawa nao wamepewa nafasi na ibara hii kwa
sifa yao ya ujuzi na uzoefu.
0784482959
0714047241

0 comments:
Post a Comment