
NA
EMMANUEL MARWA ( WAKILI
MAHAKAMA KUU).
Rasimu inayopendekezwa ili
iwe katiba inayo mambo mengi mapya.
Ni sahihi kusema mapya
kwakuwa ni mambo ambayo hayapo
katika katiba yetu tuliyonayo sasa. Moja ya mambo hayo ni hili la kuingiza au kuweka haki za
wafugaji na wakulima, wachimbaji na wavuvi. Haya ni
makundi muhimu sana katika jamii yetu
hasa kutokana na ukweli kuwa mpaka sasa kundi
kama la wakulima ndilo linaloonekana
kubeba asilimia kubwa ya watu wote katika nchi hii.
Kwa ukweli kama huu kupata
katiba au sheria ambamo haki na
mustakabali wa watu kama hawa
unatajwa si jambo la kubeza.
( a ) MALALAMIKO YA MAKUNDI YA
WAKULIMA, WAFUGAJI, WAVUVI, WACHIMBA
MADINI.
Kwa muda mrefu
sasa kumekuwepo na malalamiko
kutoka kwa makundi hasa ya
wakulima , wafugaji na
wachimba madini. Malalamiko yao makubwa wamekuwa wakiyaelekeza kwa serikali na kubwa zaidi wakiilalamikia serikali kutokuwa na sera maalum ya
kuwatengea maeneo ya kulima, malisho, kuvua pamoja
na maeneo ya kuchimba madini.
Hali hii haikuwa imeishia katika malalamiko tu bali
ilishapiga hatua na kuwa
mgogoro mkubwa ambao sasa ulikuwa
unaelekea kuwa janga la kitaifa. Na hali ilikuwa inakuwa mbaya zaidi pale makundi haya yanapoanza kugombea maeneo kwa mfano
tumeshuhudia mara kwa mara tena
katika maeneo mbalimbali ya nchi kundi la wakulima na kundi la wafugaji wakigombea maeneo.
Hali ilikuwa tete hasa
pale ilipokuwa ikiripotiwa vifo na majeruhi kutokana na magomvi
hayo. Tatizo kubwa ilikuwa ni kukosekana
kwa hiki ambacho sasa kinaelezwa
na rasimu hapa chini.
( b ) WAKULIMA, WAFUGAJI, WAVUVI,
WACHIMBA MADINI KUTENGEWA MAENEO YAO
RASMI.
Ibara ya 46 ( 2 ) inasema kuwa Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa
kisheria kwa madhumuni ya kubainisha na kutenga maeneo ya ardhi kwa ajili ya
matumizi ya kundi la Wakulima, wafugaji, wavuvi na wachimbaji madini.
Ibara kama hii ni ibara muhimu
kwa mustakabali wa uchumi na
amani ya nchi yetu.Makundi ya jamii
hizi ni makundi ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi ya ajabu.
Hatari
kubwa ambayo imekuwa ikitukabili kama
taifa ni kuwa wakati makundi ya
wakulima, wafugaji na wavuvi yakiongezeka
kwa haraka mno ardhi tuliyonayo
imekuwa ikibaki ileile. Hii ni kusema kuwa mahitaji ya ardhi yanaongezeka
wakati ardhi haiongezeki. Kwa usemi huu
kila mtu anaweza akapima hatari ambayo kama taifa tulikuwa tunaanza
kukabiliana nayo.
Ni bomu kubwa lililokuwa likijitega taratibu. Kutokana na hali kuwa
hivi ilikuwa basi
inahitajika sera madhubuti ya kudhibiti hali hii. Na sera ya kudhibiti hali kama hii haikupaswa kuwa sera ya kawaida. Ilitakiwa kuwa sera inayotokana na sheria kuu kama katiba. Na hiki
ndicho kilichofanyika.Pamoja na
hayo zipo haki nyingine za makundi haya kama
tutakavyoona hapa chini.
( c ) SASA NI LAZIMA WAKULIMA, WAFUGAJI KUPEWA TAARIFA KUHUSU
SHUGHULI ZAO.
Ibara
hiyohiyo ya 46 (b) inazidi kusema kuwa wakulima.wafugaj,wavuvi na wachimba
madini watakuwa na haki ya kupata
taarifa na maarifa kwa lengo la kuboresha kilimo, ufugaji, uvuvi na uchimbaji
madini.Hapo juu tumeona haki ya makundi
haya kutengewa maeneo maalum. Hapa sasa tunaona haki yao ya kupata taarifa ikiwa ni pamoja na maarifa.
Taarifa
maana yake ni kuwa serikali sasa
inalazimika kuweka mitandao ya kuwapasha
habari wakulima, wafugaji na wachimba madini kuhusu shughuli zao. Kwa hiyo kuwapasha
habari si hiyari tena isipokuwa lazima
maana ni takwa la kikatiba.
Kwa
upande wa maarifa ni kama kuwaaandalia
semina, majukwaa ya mijadala ya
kielimu,kuwaunganisha na shule za
kilimo,mifugo na uvuvi, vipeperushi na vijarida na kuwaandaa kwa kila kitu
kuhusu elimu. Hili nalo si la hiyari tena kwakuwa litakuwa kikatiba.
( d ) WAKULIMA, WAFUGAJI, WACHIMBA MADINI NA
HAKI YA KUMILIKI
ARDHI.
Ibara
hiyohiyo ya 46 ( a ) inawapa tena
wakulima, wafugaji,wavuvi, wachimba madini haki ya kumiliki ardhi kwa kusema kuwa (a) wakulima, wafugaji,wavuvi,
wachimba madini watakuwa na haki ya kumiliki, kutumia na kuendeleza ardhi kwa
ajili ya shughuli zao;
Kama Watanzania wengine
haki ya kutumia na kumiliki ardhi walikuwa nayo hata kabla ya rasimu hii.
Lakini sasa kuiweka katika Katiba na huku ikiwarejea wao peke yao ni jambo la mafanikio na linaloonesha
ni kwa namna gani ipo ari
ya kushughulikia matatizo yao. Pia inaonesha ni kwa kiasi gani makundi haya sasa yanatambulika rasmi na haki zao zinatofautishwa na haki za makundi mengine.
( e ) UMUHIMU AU
FAIDA KATIKA IBARA HIZI JUU.
Kuna kitu kikubwa kimoja ambacho kinajitokeza na kuwa kama faida kubwa ya ibara nilizoeleza hapa juu. Kutokana na ibara kuwa
katika mtindo huo tuliouona hapo juu
sasa ieleweke wazi kuwa makundi yote yaliyotajwa katika ibara hizi
yamepata ruhusa ya kuifungulia
mashtaka serikali iwapo lolote katika yaliyoorodheshwa kama haki zao hayakutekelezwa.
Hii ina maana baada ya
kupita kwa rasimu na kuwa katiba
wakulima, wavuvi, wachimba madini wasipotengewa maeneo maalum kwa ajili ya shughuli
zao basi
wanaweza kuishtaki serikali kwa
maombi maalum( petition) na wakapata
haki hizo ikiwemo fidia. Kwa hiyo sasa ni kusema kwamba suala la
serikali kutenga maeneo maalum kwa ajili ya makundi
haya sasa ni la
lazima.
0784482959, 0714047241
0 comments:
Post a Comment