NA
MAWAKILI WETU-
Tunapita
katika kipindi ambacho kama umakini, ukweli
na weledi utazingatiwa taifa laweza
kuwa kati ya mataifa tulivu yaliyostaarabika
katika nyanja za siasa, uchumi na jamii. Kinyume chake ni taifa la visasi,mivutano, lisilojali utu
haki za msingi na linaloendeshwa kinyume
na ustaarab wa dunia. Kulifikia hili umakini unatakiwa kutoka kila upande, upande wa watawala na watawaliwa
pia. Lakini kwa upande wa watawaliwa unahitajika umakini wa zaidi na wa ziada kwasababu upande wao ni wa kupoteza, ni upande
mbaya , upande dhaifu. Ubaya wa upande huu unatokana na sababu za kusababishiwa
na za kusababisha.Nazumgumzia za kusababisha. Watawaliwa wananchi wana utamaduni
wa miaka mingi wa kutopenda kufuatilia mambo yao wenyewe mpaka mambo hayo yawe
ajenda za wanasiasa. Leo tuna habari ya rasimu ya katiba, haishangazi kukuta kati
ya ibara 189 zilizo kwenye rasimu mtu hajawahi kuona hata ibara moja iwe kwenye
gazeti au pengine popote. Anasubiri kulalamika atakapokuwa anapata huduma mbovu
zinazotokana na kupitishwa kwa Ibara hizo.Ni rahisi na kawaida kwa baadhi ya
watu kuhisi hawahusiki, na hili
likijitokeza tena katika mchakato huu basi itakuwa hatari na msiba. Hayumkini
haitapita mda mrefu walewale walioona jambo
hili haliwahusu watakuwa wa kwanza kabla ya mwingine yeyote kugundua kuwa
walikosea sana na kuwa jambo hili lilikuwa
linawahusu tena pengine sana kuliko wale
waliofikiliwa kuwa ndio wahusika. Hata
hivyo itakuwa haina maana kwakuwa watakuwa nje ya mda( time bared) na
hakutakuwa na uwezo wa kufanya lolote isipokuwa kusikilizia maumivu tu.
Nimewahi
kujiuliza unaweza kutumia njia gani ili kuvuta umakini wa watu. Nilipata majibu
lakini sikurudhika nayo. Sikuridhika nayo kwa kuwa majibu
niliyopata yalishafanyiwa
kazi sana lakini hakukuwa na mwitikio
chanya. Ni hatari.
Mchakato
wa katiba ni maarufu sana lakini amini usiamini unahusisha watu wachache sana.Tuko
milioni 45 isikushangaze kukuta wanaofuatilia na kushiriki hawafiki hata
milioni moja. Hii ni kuanzia utoaji wa maoni , ufuatiliaji wa lililokuwa bunge
la katiba na ufuatiliaji wa jumla wa mchakato huu. Walio wengi hupenda
kuhadithiwa, au kusikiliza wadau wao
katika siasa na hufanya mawazo ya wadau
wao kuwa yao. Hupenda wanasiasa watafakari kwa niaba yao. Watu huuza tafakari
zao kwa wanasiasa, ni hatari.
Anayetaka
kubadilika anaweza kuanza sasa kwa kufuatilia safu hii ambayo itakuwa ikileta maelezo
na uchambuzi wa ibara mbalimbali muhimu katika rasimu ya katiba inayopendekezwa
mpaka mchakato utakapokwisha. Mazingatio ni kuwa uchamnbuzi huu hautakuwa wa upande wa ndio au hapana , Ukawa
au CCM isipokuwa utajikita katika hali
halisi ili itoshe na iwe fursa ya mtu kufikiria mwenyewe.
Uchambuzi utakuwa katika maelezo mepesi yenye kueleweka hasa yakilenga watu wa kada ya kati na
chini ambao haswa ndio husaidiwa na wanasiasa kufikiri. Nitakuwa
nikieleza ibara zenye maudhui
yanayofanana kwa wakati mmoja na hiyo ni
kusema kuwa leo tunaanza na Sura ya sita
Ibara za 65,66,67,68 na 69.Ibara hizi
kwa pamoja zinazungumzia Uraia wa
Jamhuri ya Muungano.
URAIA NININI.
Uraia
ni utambulisho. Wakati mwingine uraia huenda na nasaba lakini si lazima. Uraia
zaidi ni utambulisho tu, ni kuwa fulani ni wa sehemu fulani basi.Si lazima uwe
na uhusiano na uzao. Kuna tofauti kati ya unasaba na uraia. Yawezekana watu wa
nasaba moja wakawa raia wa nchi tofauti vivyohivyo watu wa
nasaba tofauti wakawa raia wa nchi
au taifa moja.Ushahidi ni Marekani. Kwa hiyo watu waelewe hili kuwa unapozungumziwa uraia hauzungumziwi udugu wa
damu bali utambulisho. Mtu aweza
kutambulika kuwa yeye kwasababu za kisheria
anatokea katika eneo la mipaka fulani, mtu huyohuyo kesho akawa mtu wa
mipaka mingine na keshokutwa mingine.
Rasimu pendekezwa imeugawa uraia au utambulisho katika makundi mawili. Kwanza uraia au utanbulisho
wa kuzaliwa pili uraia au utambulisho wa
kuandikishwa. Ibara ya 65(2)
inanukuliwa hivi “Uraia wa Jamhuri ya Muungano ni wa aina
mbili na utapatikana kwa njia ya kuzaliwa au kuandikishwa”.
Kila
moja katika haya lina mazingira yake, mwongozo wake na hadhi yake kama
inavyoelezwa hapa chini :
URAIA WA KUZALIWA.
Uraia
wa kuzaliwa umegawanyika katika makundi matatu, nayo ni :
( a ) Ni uraia unaotokana na kuzaliwa ndani ya Jamhuri ya muungano iwe
Zanzibar au Tanganyika .Uraia huu unaainishwa katika Ibara ya 67 ( 1 ). Ieleweke kuwa si yeyote atakayezaliwa katika
Zanzibar au Tanganyika ataitwa Mtanzania
isipokuwa ataitwa Mtanzania ikiwa Baba
au Mama ni Mtanzania au wote kama ni Watanzania. Ni kusema kuwa kama baba si
mtanzania wala mama lakini mtoto kazaliwa ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano
basi mtoto huyo hawezi kuwa Mtanzania. Utaona wazi kuwa ili mtu awe Mtanzania
katika hili yamezingatiwa mambo makuu mawili. Kwanza azaliwe ndani ya
jamhuri na hapohapo mmoja kati ya wazazi
wake awe mtanzania au wazazi wote wawe
watanzania. Hali hiyo ikitokea anazaliwa mtu kwa utambulisho wa Mtanzania.
( b ) Uraia mwingine katika uraia wa kuzaliwa ni pale ambapo mtu atazaliwa nje ya Tanzania na hapohapo mmoja kati ya wazazi wake awe
baba au mama au wote wawili akawa ni
mtanzania. Mwingereza aishiye Uingereza amezaa na mama mtanzania na wanaishi
Uingereza mtoto huyo ni Mtanzania. Baba
wa Kitanzania aishiye Marekani amezaa na mama wa kimarekani na wanaishi
marekani mtoto wao atakuwa mtanzania.
Baba mtanzania , mama mtanzania wote wanaishi Zambia mtoto wao atakuwa Mtanzania. Hii ndiyo maana yake
na ruhusa hii inatolewa na Ibara ya 67(
2 ).
Hizo
ndizo aina tatu za uraia wa kuzaliwa.
URAIA WA KUANDIKISHWA.
Uraia
wa kuandikishwa nao umegawanyika sehemu tatu kama ifuatavyo :
( a ) Mtu ambaye si mtanzania lakini amekuwa mkaazi wa Tanzania na kutimiza masharti ya kisheria ikiwa ataomba kuandikishwa kama raia wa
Tanzania basi ataweza kupata haki ya
kuwa mtanzania wa kuandikishwa. Ni kusema tu kuwa wageni ambao wamekaa nchini na kupata hadhi ya
ukaazi wanayo nafasi ya kuomba
Utanzania.
( b ) Mtu anaweza kuomba kuwa raia wa Tanzania wa kuandikishwa ikiwa atakuwa
amefunga ndoa na raia wa Tanzania na kudumu naye katika ndoa kwa kipindi cha
miaka saba mfululizo. Raia wa Amerika ambaye anaishi Amerika lakini kamuoa Mtanzania
na ameishi naye kwa kipindi cha miaka
saba mfululizo anayo haki ya
kuomba kuwa raia wa Tanzania. Hii haijalishi
ni kwa kuoa au kuolewa Mtanzania aliyeolewa na mme mgeni anaweza kuomba
na mtanzania aliyeoa mke mgeni anaweza kuomba.
( c ) Mtoto aliye na umri wa chini ya miaka
kumi na nane ambaye
wazazi wake si raia wa Tanzania,
akiasiliwa na raia wa Jamhuri ya
Muungano, kuasiliwa kwake, kutawezesha
mtoto huyo kuwa raia wa Jamhuri
ya
Muungano wa kuandikishwa
Huu
ndio uraia wa kuandikishwa.
MWENYE ASILI YA
TANZANIA NA AKAACHA KUWA RAIA
WA TANZANIA.
Ibara
69 ya rasimu imependekeza kitu kingine
kinacholenga kutambua baadhi ya watu . Nje ya nchi wapo watu wengi ambao ni wazawa wa Tanzania , damu yao ni ya
Tanzania lakini kwasababu mbalimbali hasa za kisheria wamelazimika kuacha uraia
wa Tanzania. Kwa mfano kuna walioolewa
na kuoa nje ya nchi na sheria za kule zikawalazimisha kukana utaifa wa nchi
kabla ya kuruhusiwa kuishi huko. Kimsingi ni wa Tanzania isipokuwa ni sheria tu imewafanya kuwa raia
wa nchi nyingine. Unakuta wana baba zao Tanzania, mama zao, dada , halikadhalika
watoto. Rasimu hii inasema kuwa hawa hawatakuwa raia wa Tanzania wala
hawatakuwa wageni kama wageni wengine isipokuwa
watapewa hadhi maalum ambayo itawatofautisha wao na wageni wengine wasio
na asili ya nchi hii. Bila shaka jambo hili limeigwa kutoka India ambako
wahindi walio nje ya India lakini wana
asili ya Uhindi hupewa hadhi maalum. Hata wahindi tunaowaona hapa kwetu wengine
wamezaliwa Ifakara,Igunga na wengine ni viongozi katika serikali , bunge na mahakama wakienda India hupewa hadhi maalum.
HADHI MAALUM NININI.
Kwanza
ni kupata kitambulisho ambacho si uraia wa Tanzania wala si kibali cha kuishi
kama anachopewa mgeni mwingine.
Pili,
hadhi maalum inaambatana na baadhi ya haki mfano kuruhusiwa kupata
elimu,kudahiliwa vyuo vya elimu ya juu, kutotakiwa kuwa na visa anapoingia na
kutoka nchini, kupata huduma nyingine za kijamii kama raia na pengine kuruhusiwa kumiliki mali
isiyohamishika kama ardhi lakini kwa kiwango chenye ukomo fulani labda eneo kidogo
kwa ajili ya makazi tu.
Aidha
kuna vitu ambavyo hawezi kuwa na haki navyo kama kupiga kura, kugombea au
kupigiwa kura, kupata ajira serikalini hususan kwenye vyombo vya ulinzi na
usalama na uhuru wa kumiliki ardhi kwa kiwango kikubwa au kisicho mipaka.
Hii
ndio maana ya hadhi maalum.
URAIA NI WA NCHI MOJA.
Ibara
ya 69 inasema kuwa uraia ni wa nchi moja. Mwanzoni ilipendekezwa uraia wa
nchi mbili kama katika baadhi ya nchi.Hili lilikataliwa na kama lingekubaliwa ingewezekana kuwa na Mmalawi,
Mtanzania, Mkenya Mtanzania, Msomali Mtanzania n.k. Kwasasa utaamua ima uwe
Mtanzania au raia wa nchi nyingine.Hakuna nafasi ya kuwa raia wa nchi mbili.
FAIDA
ZA IBARA HIZI..
Tumeona
hali ilivyo kuanzia ibara ya 65 mpaka
69, swali la ni kitu gani kimezingatiwa katika kupendekeza Ibara hizo kusomeka hivyo linajibiwa hapa chini:
( a ) Ulinzi na usalama umezingatiwa kwa mfano pale ambapo uraia wa nchi
mbili unazuiwa. Ingekuwa rahisi mtu kufanya uhalifu hapa na akaenda kuishi
kwingine ambako ana uraia sababu yuko huru. Hata kiongozi angeweza kufanya
ufisadi wa haki za binadamu au mabilioni ya hela kwakuwa ana uraia wa nchi nyingine anahamia
huko kwa amani kwakuwa huko hatafukuzwa au muda wa kibali chake hautaisha
kwakuwa ni raia. Pia kwa kiasi inaondoa uwezekano wa kuingiliwa kisiasa kwa
kupandikiza watu ambao wanalenga
kutekeleza mikakati haramu ya kijasusi inayoweza kuratibiwa na nchi nyingine.
( b )Kuondoa matabaka kwakuwa baadhi ya watu
hasa wenye uraia wa nchi mbili wangeonekana ni watu wa hadhi fulani kuliko wengine.Ni
kuzalisha tabaka jipya la Watanzania asili na Watanzania mseto. Na ni ukweli usiopingika
kuwa ni wenye uwezo wa kifedha tu ambao wangeliweza hili. Sitaki kuamini kuwa Mtanzania
anayeishi chini ya dola moja angeweza kuwa na wazo la kupata uraia wa nchi
nyingine. Kula kwenyewe shida halafu afikirie kupata uraia wa nchi nyingine,
haiwezekani. Pengo la matabaka lingekua.
( c ) Sababu za kiuchumi. Matajiri wa nchi nyingine ndio wangechangamkia
fursa hii ili wapate kutanua na kuogelea kwenye rasimali za nchi. Hakuna ambaye
angeweza kushindana nao.Wangenunua maelfu na maelfu ya ekari za ardhi na wazawa
haswa wangebaki kuwa manamba na walinzi wa maeneo hayo.Ananunua ekari alfu moja
anaweka kijumba cha chumba kimoja kwa ajili ya Mtanzania kumlindia, isingekuwa
sawa.
(
d ) Nasaba ya mtu mwenye asili
ya Tanzania imelindwa pale ambapo hata
kama yuko nje ya nchi na ameolewa au kuoa
raia wa nchi nyingine mtoto yule aweza kuwa raia wa Tanzania pia pale
inapotolewa heshima ya HADHI MAALUM. Damu ya kizalendo ya nchi imelindwa.
IMEANDALIWA NA
MAWAKILI WA BLOG HII.
0784482959
0714047241
0 comments:
Post a Comment