Saturday, 7 February 2015

KATIBA MPYA KUMALIZA USHINDI WA UBABAISHAJI UCHAGUZI MKUU





NA   EMMANUEL   NDANU  (WAKILI  MAHAKAMA  KUU)

Katika uchambuzi wa leo wa rasimu inayopendekezwa ili iwe katiba  tumeona ni vyema  kuifanyia mapitio sura ya 8 ya rasimu hii  ambayo kwa ujumla inazungumzia  pamoja na mambo mengine uchaguzi wa rais. Yako mambo mengi katika sura hii kumhusu rais au nafasi ya rais  lakini hayatazungumzwa yote isipokuwa itaguswa Ibara ya 86 ( 6 )   ambayo inazungumza hivi

  “ Mgombea wa nafasi ya madaraka ya Rais atatangazwa kuwa
amechaguliwa kuwa Rais iwapo atapata kura zaidi ya asilimia hamsini ya
kura zote halali zilizopigwa kwa nafasi ya madaraka ya Rais.”
Kwa  kipindi cha takribani miaka kumi na tano iliyopita hili kwetu halikuwako. Rais alikuwa  akipata ushindi hata kwa  kumzidi mwenzake kura moja. Ibara hii mpya katika rasimu  inaleta mfumo mpya wa kumpata rais. Ukifanya tathmini duniani utaona kuwa  asilimia kubwa ya mataifa ambayo hujinasibisha na mfumo wa demokrasia  hutumia mfumo huu  wa asilimia hamsini katika chaguzi zao.

Kwa walio wengi hapa kwetu hasa vijana hususan miaka thelathini kushuka wanaweza kuona kitu hiki kama kigeni sana katika  nchi yetu. Ukweli ni kuwa  utaratibu huu wa kumpata  rais kwa mtindo wa asilimia hamsini si mgeni. Itakumbukwa kuwa  Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977  ilikuwa na ibara ya namna hii  na chaguzi za kipindi hicho zilifanyika katika utaratibu wa  aliyezidi asilimia hamsini ndio mshindi.

Ni mabadiliko ya 13 ya Katiba ya mwaka 2000 ndiyo yaliyoondoa utaratibu huu na kuweka utaratibu  huu tulionao sasa  ambapo mtu anaweza kutangazwa kuwa rais  hata kwa kumzidi mwenzake kura moja. Hii ni kusema kuwa mtindo huu sasa unakufa tunaanza mtindo wa asilimia ambao ndio unaotumika kwa wingi hivi sasa duniani. Wapo wanaoona  mtindo tuliokuwa nao ni mzuri na wapo wanaoona mtindo mpya wa asilimia ni ndio mzuri zaidi. Inategemea na mtazamo hasa kimaslahi.

Kihistoria chimbuko la  utaratibu wa wingi wa kura kama tulionao na wingi wa kura kwa asilimia ilikuwa ni katika jitihada za wanazuoni katika kutafsiri maana ya neno KURA ZA WENGI (Majority Vote). Katika  harakati hizo baadhi ya wanazuoni wakaja na mawazo kuwa kura za wengi  ni ile idadi kubwa zaidi kuliko  nyingine  ikiwa na maana  hata  kumzidi mtu kura moja  tayari yule aliyemzidi mwenzake kura moja anahesabika kuwa  ndiye aliyependwa na wengi zaidi kwakuwa amemzidi mwenzake kura moja.

Wanazuoni wengine  wakakata wazo hili nao wakaja na wazo kuwa  wingi hauwezi kuhesabiwa hata kwa kuzidiana kura moja isipokuwa maana ya wingi wa kura  iwe ni wingi wa asilimia. Wakimaanisha kuwa  ikiwa wtakaopiga kura ni alfu moja  basi atakayepata zaidi ya  nusu ya hizo ambazo ni zaidi ya mia tano huyo ndiye atakayekuwa mshindi.Lakini ikiwa  mmoja amepata kura mia nne hamsini  na mwingine amepata miatatu kati ya alfu moja zilizopigwa basi  hata huyu wa 450 hatahesabiwa kuwa ameshinda.

Yote ni mawazo tu  ya wanazuoni ambayo ndio chimbuko la Ibara hii. Mitazamo yote yaweza kuwa sahihi au hapana au mmoja waweza kuwa sahihi zaidi kuliko mwingine. Zaidi ya hayo sisi pia  tuangalie faida na hasara za ibara iliyokaa katika mtindo huo.

FAIDA  AU   UZURI  WA   IBARA  HII.

( a ) Uzuri wa kwanza wa kuhesabu ushindi kwa mtindo wa zaidi ya asilimia hamsini ni kuwa  taswira halisi ya  mshindi kuwa ndio chaguo la wengi inajitokeza. Chaguo la wengi linakuwa linakuwa  chaguo la wengi kweli. Hii ni kwakuwa  mfumo huu katika kuhesabu mshindi unazingatia idadi ya waliopiga kura na aliyevuka nusu ya kura hizo.

 Kwa mfano waliopiga kura ni laki moja  hii ina maana ili mtu awe mshindi inabidi apate zaidi  ya elfu hamsini.Kimahesabu wingi wa watu laki moja ni kweli kabisa unahesabiwa kuanzia zaidi ya nusu yake ambao ni  elfu hamsini. Hivyo anayepata zaidi ya watu hao huyo kweli ndiye aliyependwa zaidi kwakuwa amependwa na zaidi ya nusu.

Wakati ingekuwa katika mfumo ule tunaotumia sasa ambao si wa asilimia hamsini  kama wapiga kura wangekuwa  laki moja  mgombea mmoja akapata  kura mia tano na mwingine akapata mia tano na mbili(502) na nyingine  zikaenda kwa wagombea wengine huyu wa mia tano na mbili angetangazwa mshindi bila kujali zaidi ya kura elfu tisini na tano(95000)  zilizomkataa. Kwa hiyo utaona kuwa mtindo wa asilimia  unajenga na kuleta taswira ya kweli katika kanuni ya wingi wa kura (majority vote) katika kumpata mshindi.

( b ) Faida nyingine ya mshindi kwa wingi wa asilimia ni kuwa  inaonesha kwa dhati  kiwango cha kukubalika kwa mshindi. Mfano mfumo tulionao sasa rais anaweza kuwa rais hata kwa kumzidi mwenzake kura moja tu.

Kwa hali ya kawaida  ukimshinda mtu kwa kura moja picha inayokuja ni kuwa pamoja na ushindi wa mgombea  wako wengi hawamkubali. Ina maana katika jamii iliyopiga kura mshindi na mpinzani wake wanalingana katika kupendwa isipokuwa  tofauti yao ni mtu mmoja tu ambaye pengine naye amepatikana kwa kuwa mshindi ana familia kubwa zaidi ya mshindwa.

Kimsingi hata  mshindi wa kwanza na wa pili wakitofautiana kura tano au hata kumi bado  utaona kuwa hata yule aliyemzidi mwenzake hakubaliki sana. Lakini kwa mtindo wa asilimia  hakuwezi kuwapo na tofauti ya kura moja , mbili, kumi ishirini, thelathini na pengine hata mia. Utofauti wa kura huwa ni mkubwa  kiasi cha kujenga taswira iliyo wazi kuwa mshindi anakubalika kwa  watu wengi zaidi kuliko  mwenzake.

0784482959
0714047241


                                                  
Share this article :

0 comments:

Post a Comment