Saturday, 7 February 2015

FAIDA KUU KATIKA MUUNDO MPYA WA MUUNGANO .




NA   MAWAKILI   WETU.

Ni ibara ya 70 katika rasimu  iliyopitishwa na Bunge Maalum la katiba  bila watu wajiitao UKAWA na ni Ibara ya   60 katika rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba maarufu kama tume ya Warioba. Ni ibara  ya moto sana . Wengi wamekwisha kufarikiana  na wengine wamekwenda mbali zaidi kiasi cha kutotoleana hata salamu. Sababu haswaa ya yote hayo ni Ibara hiyo.Wanagombea nini na wanajengeana chuki kwa ajili gani. Ni kwa ajili ya taifa na wanataifa ?, ni kwa ajili ya makundi yao wanayoita vyama vya siasa ?, ni kwa ajili yao binafsi  mmoja mmoja ?, ni kwa ajili gani haswa. Siri wanayo wao. Nani wa kuaminiwa kati yao, na kwa nini aaminike, kwa historia yake  au kwa analolisema  leo  jukwaani. 

Ni kazi ngumu kutegua kitendawili hiki. Anayetaka wepesi kidogo wa kutegua kitendawili hiki kanuni ni moja tu, nayo ni kuwa mfuatiliaji wa karibu sana wa  mambo  huku ukiepuka kupenda sana kusimuliwa kuliko kufanya utafiti mwenyewe.

Leo si kama jana, mambo yamerahisishwa taarifa zipo kila mahali zinamsubiri tu wakuzipekua na kuzifanyia kazi. Mitandao ya kijamii na intanet kwa ujumla wake,mawasiliano ya magazeti, redio na runinga vyote hivi  vyaweza kukupa fursa ya kuwa na fikra huru . Kwa kufanya hivyo utakuwa umejiweka mbali na kuburuzwa, mbali na ndio mzee, ushabiki usio na tija na kuwa  mbali na virusi vingine vyote vyenye kuharibu akili. Epuka kughiribiwa hasa kipindi hiki tunapoelekea kwenye kura ya maoni ya rasimu katiba .

Ibara nilizotaja hapo juu ni kuhusu Muundo wa Muungano wa Serikali ya Tanzania katika rasimu. Kawaida ya safu hii  huwa hatumshikii mtu akili  wala hatufikirii kwa niaba ya mwingine. Huwa inachukuliwa Ibara katika rasimu   inatolewa maelezo na inaelezwa faida za na hasara zake ili basi  iwe fursa kwa msomaji kutafakari mwenyewe na kujua upi mchele na ipi pumba.

SURA  YA  SABA  IBARA  70.  MUUNDO  WA  MUUNGANO.

Nukuu “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na muundo wa Serikali
mbili ambazo ni:
(a) Serikali ya Jamhuri ya Muungano; na
(b) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.” Mwisho wa nukuu.

Ieleweke kuwa mamlaka ya nchi hutekelezwa na kudhibitiwa  na vyombo vikuu vitatu. Serikali ni moja ya vyombo hivyo ambavyo vingine ni mahakama na bunge. Vyombo hivi hufanya kazi kwa pamoja  huku kanuni ya udhibiti na urari  (checks and balance) ikiwa ndio msingi wa utekelezaji majukumu ya vyombo hivi. Serikali zikiwa mbili maana yake ni kuwa na vyombo hivi vingine navyo vitakuwa Viwili viwili. Serikali ya Mapinduzi bunge lake na mahakama zake, serikali ya Tanzania bara kama inavyoitwa  nayo bunge lake na Mahakama yake. Kwa mfumo huu bunge na mahakama ya Muungano ndio bunge na mahakama ya Tanzania bara wakati bunge na mahakama ya Zanzibar  si bunge na mahakama ya Muungano. Hii ndio sura halisi ya Ibara hii kwa uwazi kabisa.

Kwa muonekano huu hakuna tofauti kati ya rasimu na katiba hii ya sasa ambayo nayo inazungumzia kitu hikihiki.Mabadiliko labda kama yatakuwa katika viunga,taasisi na namna ya madaraka katika utekelezaji wa majukumu lakini kimuundo hakuna jipya .

Yumikini kila jambo lina faida na hasara zake na ndio ada ya ukurasa huu  kuainisha baadhi ya faida na hasara ambazo zinazotokana na kuwapo kwa munndo wa aina hii. Faida au hasara zinatokana na mambo mengi ikiwemo taasisi ambazo hupatikana chini ya muundo, uongozi wake, mamlaka, uhusiano wa ndani na nje ya muungano, uhusiano na vyombo vingine vya dola kama bunge na mahakama, mgongano wa masuala ya sheria, maslahi ya wananchi ambao ndio chimbuko la mamlaka, uchumi wa nchi husika  na mengine mengi kama tutakavyoona hapa chini.

FAIDA  ZA  MUUNDO  WA  SERIKALI  MBILI.

( a ) Ni ukweli ambao hauwezi kuwa na mpinzani kuwa serikali mbili zinapunguza gharama. Lakini zinapunguza gharama ikiwa kuna pendelezo la kuwapo serikali tatu au nne. Kukiwa na pendekezo  la serikali moja  jibu haliwezi kuwa sawasawa. Upungufu wake wa gharama unatokana na ukweli kuwa  ili Muungano ufanane na miungano mingine duniani ulitakiwa uwe  na mamlaka tatu zilizo wazi , mamlaka huru ya muungano , mamlaka huru ya Tanganyika na Mamlaka huru ya Zanzibar. 

Badala yake mamlaka zinakuwa mbili  ya Tanganyika na Zanzibar huku ya Tanganyika ikiingia katika ile mamlaka ya muungano na kuwa moja hivyo kuua mamlaka moja na kubaki mbili. Mamlaka tatu maana yake ni kuwa kila mamlaka na kiongozi wake mkuu awe rais au waziri mkuu, kiongozi mkuu msaidizi, itifaki ya ulinzi inayojitegemea, vyombo vya usafiri vinavyojitegemea magari ya kutosha , ndege, ofisi kubwa zenye hadhi na zinazojitegemea, watumishi wa kila idara na kila kitu ambacho kinahitajika kwa sehemu kuitwa mamlaka ya dola. Hizo zote tunaongelea fedha. 

Hakuna maelezo hapo ni fedha tu .Kwa serikali mbili maana yake ni kuwa vitu hivi vinagawanyika mara mbili tu na itifaki zote nilizotaja hapo juu zinakuwa mara mbili badala ya tatu na hivyo kuweka wepesi katika gharama.

( b ) Serikali mbili zinaweka mbali uwezekano wa kuvunjika kwa muungano. Muungano unapokuwa wa mkataba au serikali tatu  inasogeza karibu uwezekano wa kuuvunja muungano hasa kutoka kwa viongozi ambao wanaweza kujitokeza wakiwa na fikra na sera zenye mrengo huo. 

Muungano wa serikali mbili  unapunguza sana uhuru wa washirika katika kuamua mambo yao  hasa upande wa Zanzibar  kitu ambacho kinalazimisha  kuwapo kwa muungano. Kwa mfano kwa muungano huu serikali ya Zanzibar haina uwezo wa kuamua kuwa sasa tunajitoa katika muungano kutokana na namna  muungano wenyewe ulivyoundwa. Lakini kwa uhuru  wa kimuundo wa serikali za mkataba au serikali tatu jambo hili linawezekana kwa urahisi kwakuwa  aina za muungano wa aina hiyo huwa inatoa mwanya wa kufanya hivyo.Kila upande huwa unakuwa na uwezo wa kimustakabali katika kuendelea na muungano au kutoendelea. 

Huu wa serikali mbili hautoi mwanya huo. Miaka ya sabini ilikuwa rahisi kulimaliza shirikisho la Afrika ya Mashariki kwakuwa miungano ya shirikisho hutoa nafasi hizo. Shirikisho huwa ni makubaliano tu kama yalivyo makubaliano mengine yote anayeona  kabanwa anaachia kwakuwa katika makubaliano hayo huwa lazima kuwe na vipengele vyanavyohusu namna ya kujitoa. Hivyo niseme tu kuwa  muungano wa serikali mbili hivihivi zilivyo bila kugusia lolote kuhusu   upande mmoja kukaliwa au kutokaliwa unatoa nafasi ya lazima katika kuwepo kwake.  Unalazimisha maisha yake.

( c ) Pia kwa kuweka serikali mbili Ibara hii inawaweka karibu zaidi watu wa Zanzibar na Tanganyika. Ibara inawaweka karibu zaidi kwa kulinganisha na serikaki tatu au mkataba na si kwa kulinganisha na serikali moja ambayo ndiyo ingewaweka karibu zaidi kuliko zote. Panapokuwa na serikali tatu au mkataba  wazo linalojengeka ni kuwa  mnashirikiana tu kama ambavyo mnaweza kushirikiana na Kenya na Uganda au kama ambavyo mnaweza kushirikiana na Marekani au nchi nyingine yoyote. Ile hali ya kuwa  hamshirikiani isipokuwa nyie ni ndugu na mnayofanya ni kwa ajili ya udugu taratibu inaanza kutoweka. 

Mnakuwa kama majirani wengine wowote na lile fungamano(commitment) la kuwa  nyie ni ndugu linatafunwa mpaka kufikia kuwa washirika wa kawaida kabisa. Ushirika ni mwepesi na unapunguza umakini (seriuosness) katika kujaliana (careness). Muundo wa serikali mbili unaondoa  hali ya ushirika wa kawaida.
  
0784492959
0714047241

Share this article :

0 comments:

Post a Comment