Saturday, 7 February 2015

KINGA DHIDI YA MASHTAKA YA RAIS KUMFANYA RAIS AJAYE KUJIAMINI KUSHUGHULIKIA UFISADI.



NA  JACKLINE  MAJURE  (WAKILI  MAHAKAMA   KUU)

Ibara ya 93 katika rasimu inayopendekezwa ili iwe katiba  inasema hivi 93.-(1)” Wakati Rais akiwa madarakani, hatashtakiwa wala mtu yeyote
hataendesha mashtaka ya aina yoyote dhidi yake mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai”.

Ni aina ya ibara ambayo inatoa kinga kwa mtu atakayekuwa ameshika madaraka  ya rais kutoshitakiwa. Katika ibara hii kuna  mambo matatu ya kuzingatia, Kwanza kabisa ibara hii inazungumzia  wakati rais anapokuwa madarakani yaani wakati  yuko ikulu ndo asifunguliwe  mashtaka, lakini pili mashtaka yenyewe ambayo hapaswi kufunguliwa ni yale  Mashtaka ya kijinai tu ambayo ni kama kuua, kubaka, kulawiti,kupiga, kuiba, rushwa, uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya ofisi n.k. Tatu sehemu anapozuiwa kushtakiwa ni mahakamani  wala si bungeni.

Kwa kawaida viongozi wakuu hasa marais wakati mwingine hushtakiwa mahakamani au bungeni lakini kwa hapa  imezuiwa kumshtaki makahamani wala si bungeni.Kwahiyo ibara hii ndogo ya ( 1 ) imeundwa na mambo hayo matatu.

Aidha Ibara hiyohiyo Ibara ndogo ya (2) inasema hivi  “Wakati Rais ameshika madaraka kwa mujibu wa Katiba hii,haitaruhusiwa kufungua mahakamani shauri la madai kuhusu jambo lolote alilolitenda au alilokosa kulitenda yeye binafsi kama Rais ama kabla au baada ya kushika madaraka ya Rais, ila tu kama angalau siku thelathini kabla ya shauri  kufunguliwa mahakamani, Rais atapewa au ametumiwa taarifa ya madai kwa  maandishi kwa kufuata utaratibu utakaowekwa kwa mujibu wa sheria, na taarifa  hiyo ikiwa inatoa maelezo kuhusu chanzo cha shauri hilo, kiini cha madai  yenyewe, jina lake na anwani ya mahali anapoishi huyo mdai na jambo hasa   analodai”

 Ibara hii inatoa nafasi kwa rais aliye madarakani kushtakiwa kwa makosa ya madai. Ile ibara ya kwanza ya juu inakataza kumshtraki kwa makosa ya jinai wakati akiwa madarakani. Hii sasa inaruhusu kushtakiwa hata akiwa madarakani lakini kwa makosa ya madai tu. Makosa ya madai ni kama kugombea mashamba,viwanja au nyumba, kukopeshana vitu vya thamani kama fedha na kushindwa kulipa, kudai fidia baada ya kutukanwa au kudhalilishwa,kuvunja mkataba kama mikataba ya mauziano ya vitu kama magari n.k. Hayo ndio makosa  ya madai ambayo rais hata akiwa madarakani waweza kumshtaki nayo.

Aidha jambo jingine la tofauti limejitokeza  katka ibara hiyohiyo  ya 93 ibara ndogo ya (3) ambayo inasema hivi “ Isipokuwa kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na kuondolewa madarakani na Bunge, haitakuwa halali kwa mtu kumshtaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au la madai dhidi ya mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo
alilofanya wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya Rais”.

Kwanza tuliona hairuhisiwi kumshtaki rais kwa kosa lolote la jinai pale anapokua madarakani, pili tumeona inaruhusiwa kumshtaki rais kwa kosa la madai hata akiwa madarakani na sasa tunaona kuwa itakapotokea bunge limemwondoa rais madarakani  basi hakuna ruhusa mtu  au chombo chochote kumshtaki rais kwa kosa lolote liwe la jinai au la madai alilofanya akiwa madarakani.

 Sura ya jumla ya ibara hizi zote kwa pamoja ni kuwa kwanza rais hashtakiwi kwa kosa lolote la jinai  iwe pale anapokuwa madarakani au hata baada ya kutoka. Makosa yote ya jinai aliyoyafanya wakati akiwa ikulu hayaguswi kabisa. Pili ni kuwa  anayetaka kumshtaki rais kwa kosa la madai amshtaki akiwa bado yuko madarakani lakini akishatoka basi huwezi tena kumshtaki hasa kama ametoka kwa kuondolewa na bunge. Tuangalie faida au uzuri wa ibara hizi na mapungufu au hasara zake.

FAIDA AU UZURI WA IBARA HIZI

( a ) Kwanza  unapomwekea kinga rais hasa anapokuwa madarakani ambao ndio wakati wa kutekeleza majukumu yake unakuwa umempa  uhuru na umemwondolea woga katika kuamua na kutoa maamuzi magumnu  katika  utekelezaji wa sera.

Rais anafanya mambo bila woga wala bila kuhofia lolote jambo ambalo likitumiwa vyema laweza kutoa fursa kwa kushughulikia mambo sugu yaliyoshindakana kama ufisadi hasa katika kuwashughulikia wale watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha au kimamlaka ambao hufanya matendo maovu kwa kujiamini kutokana na kujijenga katika mitandao ya siasa ambayo wakati mwingine hutishia hata mamlaka ya rais.

( b ) Pili unapoweka ugumu katika kumshtaki rais akiwa madarakani  hakika unakuwa unajenga msingi wa amani na utulivu. Kurahisisha kumshtaki rais  kama raia wa kawaida kunaweza kupelekea mashauri ya mara kwa mara dhidi yake kitu ambacho kinaweza kuliyumbisha taifa kutokana na unyeti na ukubwa wa nafasi yenyewe.

0784482959 , 0714047241



Share this article :

0 comments:

Post a Comment