Saturday, 7 February 2015

KATIBA MPYA, MGOMBEA HURU KUKUZA DEMOKRASIA TANZANIA



NA  JACKLINE MAJURE ( WAKILI  MAHAKAMA  KUU)

Ibara ya  216.-(1)  katika rasimu inayopendekezwa  ili  iwe katiba  kama itapita  inasema kama  ifuatavyo  Bila kuathiri masharti ya Ibara ya 88 na Ibara ya 140, mtu atakuwa na haki ya kuwa mgombea huru katika uchaguzi unaosimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi.

Ni kwa maana hii  kuwa  ule utaratibu  wetu  wa kuwa  kila mgombea  ubunge au urais  au udiwani  ni lazima awe ametokana na chama chochote  cha siasa  utakuwa umekufa. Haufi  kwa maana kuwa vyama sasa  vimepigwa marufuku hapana,  isipokuwa  si lazima kupitia chama cha siasa ili mtu awe kiongozi  kwa  njia ya  kuchaguliwa.

 Mgombea huru atakuwa  ni mgombea ambaye hatokani na chama chochote cha  siasa na ataweza  kugombea  ubunge udiwani na hata  mamlaka makubwa ya urais  ataruhusiwa  kugombea. Pia ugombea huru umeainishwa kama sifa maalum kwa mtu ambaye  havutiwi  na siasa za vyama katika kugombea ubunge. Ibara  ya 140( 1 ) inasema hivi  

“Bila kuathiri masharti yaliyomo katika Ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge endapo:

(a) ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja wakati wa kugombea;


(b) anajua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kingereza; na


(c) ni mwanachama aliyependekezwa na chama cha siasa au mgombea HURU.


Baada ya kutimiza sifa  zilizoainishwa ambazo ni  kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano,  kujua kusoma  na kuandika  kati  ya  lugha  ya  Kiswahili  ama kiingereza lakini  basi  mtu asiye  na chama chochote cha siasa   anaweza  kuomba  ridhaa  ya wananchi ili awe mwakilishi wao bungeni.  Kwa mamlaka ya rais Ibara ya 88  baada ya sifa nyingine kutimia  imetoa ruksa  kwa mgombea huru  kuwania mamlaka hayo  kama ifuatavyo ; 

88.-(1) Mtu atakuwa na sifa ya kuchaguliwa kushika nafasi ya madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ikiwa:

(a) ni raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano


(f) ni mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa au mgombea   HURU.



Aidha katika yote hayo  ibara ya 143.-(1) inaibua  kitu kingine  kuhusu mgombea binafsi kama inavyonukuliwa hapa, “Mbunge atakoma kuwa Mbunge ikiwa litatokea lolote kati ya mambo yafuatayo:

(h) Mbunge aliyetokana na mgombea huru, atajiunga na chama chochote  cha siasa”


Kawaida tumezoea kusikia  diwani,mbunge au rais akiacha  chama  chake cha siasa anapoteza hata mamlaka yake. Ni kwasababu hii tumeshashuhudia mara nyingi baadhi ya viongozi wa siasa  wakikimbilia mahakamani kulinda nyadhifa zao baada ya  kutishiwa uanachama wao kwenye  vyama vyao  vya siasa.  Kwahiyo kama zamani  kuacha uanachama ilikuwa ndio upoteze mamlaka sasa   hata kuingia uanachama  nako  kutampelekea mwanasiasa kupoteza mamlaka.  Kwa ufupi tuangalie  faida na hasara   za mgombea huru  katika  ibara hizi.

FAIDA   ZA  MGOMBEA  HURU

( a ) Kwanza imepanua wigo wa demokrasia kwa  kuwashrikisha  watu wengi zaidi  katika  kuomba ridhaa ya nyadhifa  mbambnali. Wako watu wengi ambao walikuwa wakitaka  nyadhifa za siasa lakini hawapendi  siasa  za vyama. Kwa  ibara hii ni kusema kuwa hawa  nao wameingizwa katika kinyanganyiro  na hivyo sasa ushiriki utaongezeka.

( b ) Mgombea  binafsi atongeza ushindani  hasa majimboni. Wako watu ambao walikuwa na uwezo mzuri wa  kuwa  viongozi na wanakubalika  sana  kwa wananchi  lakini wanaenguliwa  katika kinyanganyiro  kutokana na hila ndani ya vyama. Kwa kuwapo mgombea  huru  itakuwa  chama kikimuengua mtu  anayekubalika  kwa wananchi  basi kijiandae kupambana naye  kwa ushindani mkubwa  katika uchaguzi.

( c )Itapelekea kupatikana  viongozi wenye uwezo  kiuongozi na si kiongozi mwenye  uwezo kimtandao  wa siasa. Mara nyingi viongozi wanaopatikana kupitia vyama vya siasa ni wale wenye  mitandao madhubuti katika vyama hivyo  na si wale wenye uwezo  kuiongozi. Hili wala sio siri  viongozi wetu wengi  wamepatikana kwa nguvu za mitandao hasa mitandao fedha  na si uwezo binafsi kiuongozi

0784482959,      0714047241




Share this article :

0 comments:

Post a Comment