Saturday, 7 February 2015

TUJIHADHARI NA MATUMIZI YA DEMOKRASIA, KATIBA MPYA



NA  EMMANUEL  NDANU (WAKILI  MAHAKAMA  KUU)

Sura ya pili, sehemu ya pili  ibara ya 12( 1 ) ya rasimu inayopendekezwa kuwa katiba  inasema kuwa
“Lengo la Katiba hii kisiasa ni kudumisha demokrasia”.
Rasimu inayasema haya ikiwa katika harakati za kuelezea malengo ya taifa ya kisiasa.Kimsingi  katika rasimu yako malengo ya taifa ya kijamii( social vision), malengo ya taifa ya kiutamaduni( cultural vision), malengo ya taifa ya kiuchumi( economic vision) na malengo ya taifa  kisiasa( political vision) ambayo  ndio  tunayaangalia sasa.

Ukisikia malengo ya taifa kisiasa au kijamii maana yake ni mwelekeo  wa taifa  kisiasa au kijamii. Mwelekeo maana yake ni kuwa  kila kitakachokuwa kinafanyika nchini lazima kiwe kinafanana na kile kilichosemwa  katika katiba. Taasisi zote za  dola na za kiraia   lazima zihakikishe shughuli zake zote zinafanana na lengo la kisiasa katika katiba. Na kwakuwa lengo la kisiasa ni demokrasia basi  kila taasisi ya kidola au binafsi lazima ihakikishe  shughuli zake zinafanana  na demokrasia.

Hii maana yake ni kuwa  demokrasia itakuwa ndio kioo. Taasisi au mtu binafsi atakuwa anatakiwa kujitazama  na kuona kama anafanana na  demokrasia iliyosemwa katika katiba ambapo akiona anafanana  basi hiyo shughuli anayoifanya ni halali  kwakuwa ina baraka za katiba na akiona haifanani basi shughuli hiyo ni haramu na yuko katika hatari ya kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kukiuka katiba.

Ni sawa na kusema  kuwa demokrasia kiwe ndio kiigizo chetu, iwe ndio mfano wetu.Hiyo ndio maana ya demokrasia kuwa lengo la taifa kisiasa. Kwa maneno kama haya utaona ni kwa namna gani demokrasia imetukuzwa  na kupewa hashima ya pekee kiasi cha kupendekezwa kuwa kiigizo kwa Watanzania zaidi ya milioni 45.

 Hii demokrasia nini mpaka ipate heshima kubwa kiasi  cha  kuwa lengo kuu,kiigizo kikuu, mwelekeo mkuu, na mfano mkuu  wa watu zaidi ya milioni 45 kitaifa.     

DEMOKRASIA   NININI.

Ziko tafsiri nyingi na maarufu za demokrasia ambazo wengi wetu  tunazijua. Sitaeleza tafsiri yoyote katika hizo isipokuwa nitaeleza wazo la jumla kuhusu hiki kitu kinachoitwa demokrasia ambacho  katiba yetu mpya  imetuelekeza kukisujudia.

Ukitaka kumweleza  mtu wa kawaida kabisa maana  ya demokrasia mwambie hivi, demokrasia ni haya maisha unayoyaona sasa,watu wanavaa wanavyotaka, watu wanatembea kulala na kula wanavyotaka, mtu anaamua awanie uongozi au hapana, mtu anaamua  nani awe kiongozi wake na nani asiwe, mtu anaoa au kuolewa na anayemtaka, mtu  anamkosoa anayemtaka awe kiongozi wake mkuu  au mdogo, mtu anazungumza anavyotaka , mtu anaruhusiwa kuishi popote na bila kubughudhiwa, yaani kwa  ufupi kila uhuru wa kutenda jambo unaouona hiyo ndio demokrasia.Mtu atakuelewa vyema.

DEMOKRASIA  NDIO  UBEPARI

Matendo ya kufanya mambo kwa uhuru yameanza mamilioni ya miaka iliyopita isipokuwa hayakuwa yakiitwa demokrasia. Walioanzisha demokrasia walichukua baadhi ya  matendo huru wakayaingiza katika huo mfumo wao wakayaita demokrasia.

 Lakini matendo kama uhuru wa kuongea(maoni), kutembea , kuvaa n.k yalikuwapo kabla ya kitu kiitwacho demokrasia na umri wa matendo haya waweza kuwa sawa na umri wa mwanadamu duniani.Aidha demokrasia hii tuliyonayo leo imeanza karne ya 15  kipindi cha hatua ya kwanza ya ubepari( mechantalism) na imekua mpaka hatua ya sasa ya ubepari  ambayo huitwa ubepari uliokomaa(monopoly capitalism).

Kimsingi demokrasia ndio sera kuu ya ubepari na neno demokrasia limeanzishwa na mabepari.  Kwa maana hiyo tunapoamrishwa na katiba kuwa demokrasia iwe ndio  kiigizo, chetu, na mfano wetu tunaambiwa kuwa kiigizo, na mfano wetu uwe ubepari.Ubepari(Capitalism) ndio unaomiliki kitu kiitwacho demokrasia hili wala halina shaka. Kwa ibara hii maana yake ni kuwa mwelekeo wa nchi hii ni ubepari na nchi hii sasa ni ya kibepari rasmi.

MATATIZO  YA  KUFUATA  UBEPARI.

( a ) Ielewewke kwamba ubepari ni mali ya watu na bila shaka walioanzisha na kumiliki mali hiyo wanayo malengo yao. Miaka ya nyuma kiongozi wa ubepari alikuwa Wingereza na sasa kiongozi wa ubepari ni Marekani. Wakati Wingereza akiongoza ubepari alitumia nafasi hiyo  hasa kwa mgongo wa demokrasia  kuingia Afrika na kuitawala Afrika akishirikiana na wenzake wa ulaya.

Walijifanya wamekuja  na mfumo mpya wa uongozi ambao ungeweza kumaliza matatizo  na shida za watu huku wakijua na kuamini kuwa  mfumo huo wenyeji wasingeweza kumudu misingi yake kutokana na elimu na weledi mdogo na hivyo kujikuta wameangukia mikononi mwa wageni.Kwa ufupi tuliweza kutawaliwa kwa urahisi kutokana na kuzidiwa na mbinu za hiki kinachoitwa demokrasia.  

( b ) Leo Amerika ameweza kuwa na amri juu ya dunia kupitia hiki kitu kinachoitwa demokrasia. Mila na tamaduni za asili ambazo zimezaa maadili mema na mwenendo mwema katika jamii zetu kwa muda mrefu zimekufa  na zimeuliwa na hiki kiumbe demokrasia.Tunashuhudia mavazi ya hovyo,vitendo  vya ukahaba, ushoga, heshima kutoweka kwa mkubwa na mdogo, usagaji, na ghasia nyingine nyingi kwa mgongo wa huyu demokrasia.

( c ) Wameandaa vitu wakaviita misingi mikuu ya demokrasia huku wakiamini kuwa hakuna yeyote atakayeweza kufaidika   na vitu hivyo isipokuwa wao. Mfano, moja ya msingi wa demokrasia ni kuwa na uhuru katika uchumi au uchumi huria. Katika uchumi huru ndimo penye uwekezaji  kimataifa.

Ndani ya uwekezaji wa kimataifa ndimo  ilimo fursa ya wao kuja kuogelea katika rasilimali zetu. Walijua uhuru  katika uwekezaji wa kimataifa hakuna mwafrika atayekuwa na uwezo wa kuwekeza kitu cha maana kwao. Isipokuwa wao ndio wataokuja kuvinjari ndani ya migodi yetu,maziwa yetu, bahari, mafuta, gesi, na kila kitu.Demokrasia ni mali ya watu  na wenye nayo wanayo malengo yao.

Tunatoa uhauri kuwa pamoja  na maono  mazuri ya  katibas  mpya katika kukuza  na kuimarisha  demokrasia  tunapenda  kusema  kama alivyosema  aliyekuwa rais  wa Libya  marehemu Kanali Muammar Gaddafi  kuwa demokrasia  nzuri  ni ile isiyoharibu mila desturi za wenyeji  pia  ni ile isiyotumka  kuingiza fikra za kinyonyaji.

0784482959
0714047241

                                          
Share this article :

0 comments:

Post a Comment