Rasimu
inayopendekezwa ili iwe katiba imebeba mambo mengi mazuri. Yumkini yanayojulikana ni machache.
Kwanini, sababu I wazi, ni ajenda za
kisiasa. Mambo mengi yamepigwa kumbo na
kumezwa na mambo machache sana. Mambo yahusuyo madarak na ni mifumo ya nchi yamekuwa ndio rasimu.
Rasimu
ina ibara 189, ni Ibara zisizofika hata kumi zinazopigiwa kelele. Ni masikitiko
makubwa kwakuwa zaidi ya ibara 170 zimetelekezwa, ni ibara yatima.Katika kupingana
na hilo blogi hii inaeleza na kuchambua Ibara mbalimbali za msingi sana ambazo kwa namna moja au nyingine hazitamkwi katika
ufalme wa wanasiasa. Ni leo tena ambapo tutagusa Ibara za 46, 47 na 33.Kwa
pamoja Ibara hizi zinazungumzia haki ya mtuhumiwa anapokamatwa au kuwa kizuizini,
na haki za wafungwa. Ni ibara muhimu sana.
MTUHUMIWA NI NANI.
Mtuhumiwa
ni mtu anayehisiwa kuhusika katika uhalifu wa kijinai na akawa chini ya ulinzi
katika mamlaka za kiusalama, mahakamani ikiwa kesi yake inaendelea au nje kwa dhamana huku kesi ikiendelea.Hakuna
mtuhumiwa isipokuwa lazima kuna jinai. Madai hayana mtuhumiwa yana Mdaiwa au
Mlalamikiwa.Hivyo basi Ibara hizi zikizungumzia mtuhumiwa zinazungumzia jinai.
MFUNGWA NI NANI.
Aidha
Mfungwa ni mtuhumiwa ambaye kesi yake imesikilizwa imeisha na amepatikana na
hatia katika makosa yote au baadhi na sasa ameanza au tayari anatumikia
adhabu.Hakuna mfungwa kabla ya hukumu na adhabu. Wanaozuiliwa katika magereza
na hali hawajahukumiwa na kutangaziwa adhabu hao ni watuhumiwa au rumande(remandee).
HAKI
ZIPI ZIMETOLEWA
KWA MTUHUMIWA NA MFUNGWA.
( a )Imeelezwa kuwa mtu aliyekamatwa na kuwekwa kizuizini anayo haki ya
kuelezwa katika lugha anayofahamu sababu za kukamatwa,haki ya kukaa kimya na
madhara au matokeo ya kuzumgumza lolote . Kimsingi hii si haki ya kuwa umepewa isipokuwa ni haki iliyo moja
kwa moja (automatic right). Inawezekanaje umweke chini ya ulinzi mtu
halafu umzungumzishe lugha asiyoifahamu.
Ni kwanini sasa umemweka chini ya ulinzi na unategemea lipi kutoka kwake hali
hamfahamiani kwa lugha.
Ukiangalia
unaona kuwa ni haki ambayo hata
isingesemwa ilikuwa ni lazima iwe hivyo. Na kimsingi ndivyo ilivyo hata kabla
ya hii rasimu. Ni kwanini sasa hili jambo liko hivi hata kabla ya rasimu na linaigizwa tena katika rasimu katiba.
Ni kuwa jambo hata kama ni dogo au lipo na huwa linafanyika kwa mazoea au kwa
sheria nyinginezo likiingizwa kwenye katiba hupata umuhimu maalum wa pekee na huleteleza wajibu
wa kisheria kwa maana kuwa wapo watakaoanza kuwajibika kwalo. Msingi wa kuelezwa katika lugha anayoifahamu mtuhumiwa
katika rasimu umeshikamanishwa katika
vipengela vitatu.
Kwanza kumueleza mtu kwa lugha anayoifahamu Sababu
za kukamatwa kwake, Pili haki ya kutotoa maelezo yoyote na Tatu
athari,madhara au matokeo ya kutoa maelezo au kusema lolote.
Hii
ni kuwa mtu aambiwe kwanini amewekwa
chini ya ulinzi . Habari za twende utajua kituoni hakuna.Sema mimi ni fulani
ninakuweka chini ya ulinzi wewe fulani kwasababu unatuhumiwa kwa wizi wa silaha,
kubaka , kufanya fujo n.k. Pili una haki ya kukaa kimya kama utaamua kufanya
hivyo kwakuwa hatukulazimishi kuongea lolote, na tatu aambiwe mtu kuwa lolote utalolisema kuanzia
sasa litakuwa ushahidi na litatumika katika mahakama kama ushahidi
wakosa unalotuhumiwa nalo.
Hii
ndio madhara,athari au matokeo ya kusema lolote. Athari, madhara au matokeo ya
kusema lolote ni kile ulichokisemsa kutumika mahakamani kama ushahidi, basi.
Hivyo ni kusema kuwa utatakiwa uelezwe hayo matatu katika lugha unayoifahamu kama
u mtuhumiwa.
Askari
akimweka chini ya ulinzi mzungu asiyejua Kiswahili na mzungu akakubali lakini akazungumza maneno
fulani ambayo ni ushahidi mzuri kwa alichowekewa chini ya ulinzi, maneno hayo
pamoja na uzuri wake katika ushahidi hayataweza kutumika dhidi yake kwakuwa
hakuwa ameelezwa haki hizi kwa lugha anayoijua wakati wa kukamatwa kwake.Vivyo
hivyo kwa masai asiyejua Kiswahili na wengineo.
( b )Haki nyingine ni kuwa `mtuhumiwa au mfungwa anapokamatwa na kuwa
kizuizini anayo haki ya msingi ya kuwasiliana na wakili wake au mtu mwingine
yeyote ambaye kwake anaweza kutoa
msaada. Kama ni kituo cha polisi au
pengine popote ni lazima basi wahusika wamwezeshe waliyemkamata kuwasiliana na
watu wake.
Hii
ni pamoja na kumpatia mawasiliano kama hana namna ya mawasiliano au kama hakuna kabisa uwezekano wa
mawasiliano eneo hilo basi waliomkamata wanawajibika kufika
kimwili au kutuma ujumbe panapohusika ili mtuhumiwa au mfungwa aweze kuwasiliana na mtu
aliyemtaka. Ile habari ya huruhusiwa kuongea na mtu yeyote kwakuwa uko chini ya
ulinzi mara eti unaweza kuharibu upelelezi hakuna.
( c ) Kutolazimishwa kutoa maelezo ya
kukiri kosa. Mchezo huu mahala pake haswa ni vituo vya polisi. Hutumika nguvu
nyingi kumlazimisha mtuhumiwa akiri kosa ikiwa ni pamoja na kumtesa.Upo
ushahidi mwingi watu wamerushwa kwa umeme, wameingizwa chupa sehemu za siri, kutandikwa
mijeredi hiyo wala siyo adhabu tena siku
hizi, kuninginizwa kichwa chini miguu juu
na mateso mengineyo ya kuudhi na kudhalilisha kabisa.
Pia
kumwambia mtu kwa kumshawishi kuwa sema ukisema ukweli nitakusaidia utoke au
nitakufutia kosa na mtu akalazimika kusema kama mwanausalama anavyotaka ili
ajinasue nako ni kumlazimisha kukiri kosa kwa mujibu wa ibara hii. Ili isiwe
kulazimishwa huna haja ya kumshawishi mtu, yatosha kumweleza kosa na kumuuliza
kama analikubali au kulikataa.
( d ) Haki ya kufikishwa mahakamani haraka na mapema iwezekanavyo. Mahakama
ndio hutoa haki kwa kusema huyu anakosa
au hana. Polisi,polisi jamii, mgambo , raia wema kazi yao ni moja tu kukamata
na kumfikisha mahakamani. Hawaruhusiwi kukaa na mtuhumiwa kwakuwa kisheria
wakishamkamata hawana kazi naye.
Kazi
gani watafanya naye baada ya kumkamata, haipo. Hali hii ndo inalazimisha mtuhumiwa kufikishwa haraka mahakamani . Kama
ni maeneo ya mijini au sehemu ambapo mahakama ipo karibu ndani ya masaaa 24
yatosha mtuhumiwa kufikishwa mahakamani, na kama ni vijijini , kama mtu
anakamatwa leo, siku hiyohiyo au kesho
kutokana na hali usafiri mtuhumiwa asafirishwe mpaka ilipo mahakama.
( c ) Haki ya kuwekwa katika mazingira yanayozingatia haki za binadamu. Sero
zenye mikojo na vinyesi,wadudu wachafu wa kila aina, sasa zitakuwa haramu.
Imezoeleka hivyo mpaka sasa watu wanajua kuwa maana ya kuwekwa ndani ni ukutane
na mazingira magumu ili ujutie kosa.Eti hiyo ndio ndani(sero). Sivyo hata
kidogo, kuwekwa ndani ni kusubiria tu taratibu za kisheria ambako hakuna
uhusiano na kuwekwa sehemu chafu. Inawezekana mtuhumiwa kukalishwa hata kwenye sofa na vigae kwani haiharibu chochote,
haiingilii upelelezi, wala haitamfanya ashinde au ashindwe mahakamani. Sehemu
chafu ni tabia mbaya za kinazi (Nazism),mateso na kutojali haki za watu.
( e ) Mtu anayetumikia kifungo anayo haki pia ya kupatiwa nakala ya hukumu
na mwenendo wa kesi yake ili basi imwezeshe kukata rufaa kama yu tayari kufanya hivyo au
kuchukua hatua nyingine atakazoona ni stahiki na zenye kufaa.Gharama za
upatikanaji wa nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi haziko juu ya mfungwa isipokuwa
mamlaka zinazomshilikia ndizo zitahusika na hili. Hii ni kwasababu hukumu na
mwenendo wake hupatikana kwa gharama
mahakamani.Haki nyingine za mfungwa ni kama nilivyozieleza hapo juu.
FAIDA KATIKA IBARA
HIZI.
(
a ) Awali ya yote ni kuwa
baadhi ya mambo hayakuwa katika katiba lakini
yalikuwa yakifanyika sawasawa kabisa na rasimu inavyoeleza. Umuhimu ni
kuwa mambo hayo sasa yatakuwa rasmi na tutayapata katika katiba kama itapita.
Umuhimu wake nini. Jambo linapoingia katika katiba linapata hadhi ya pekee na
linaibua ulazima katika wajibu wa kulitekeleza.
Mathalan tumeona hizo haki juu , hii ina maana
kuwa mtuhumiwa au mfungwa ambaye atatendewa
kinyume anayo haki sasa ya kufungua shauri la madai na kudai fidia jambo ambalo
lisingewezekana kama mambo haya hayapo ndani ya katiba. Kama ni magereza
anamfungulia shauri mtu hasa aliyemtendea kinyume, anaiunganisha magereza na
mwanasheria mkuu wa serikali na kama ni
polisi anamweka askari hasa aliyemtesa, analiunganisha jeshi la polisi na
mwanasheria mkuu wa serikali.
Kwa
kuwashitaki wahusika mateso yanaweza kupungua kwakuwa serikali itajikuta
ikilipa mamilioni ya fedha kama fidia mara kwa mara. Kwahiyo wakuu wa usalama
watawatahadharisha watendaji wao ili kuepuka migogoro na kunusuru mamilioni ya shilingi.Hii ni kusema kuwa kuteswa sasa
yaweza kuwa kazi nzuri yakupatia mtaji
au kutoka kimaisha.
( b ) Pia inaposemwa kuwa mtuhumiwa au mfungwa aelezwe shitaka au mwenedo wa
kushauri kwa lugha anayoifahamu hili linakwenda
mpaka katika nakala ya hukumu. Sheria ya sasa lugha ya mahakama hasa
kuanzia mahakama ya wilaya ni kiingereza. Hii ni katika kuweka kumbukumbu
lakini mambo mengine inatumika lugha wanazofahamu wahusika. Inaposemwa lugha ya
kumbukumbu ni kiingereza ina maanisha kuwa hukumu zote na mienendo lazima iwe
kwa kiingereza.
Kwa
ibara hii utawekwa utaratibu sasa au yatafanyika mabadiliko ili kuwawezesha
wafungwa na wengine kupata nakala za
hukumu kwa lugha wanazofahamu hususan Kiswahili. Ni jambo jema kwakuwa ilikuwa
mtu akipata nakala ya hukumu lazima amtafute mkalimani.
( c ) Haki nyingine ni mfungwa na mtuhumiwa kukaa mazingira safi na
salama ambalo limekuwa jambo la msingi
kwakuwa limezingatia ubinadamu. Niseme jambo moja tu kuwa haki ya ubinadamu yaani
kwamba fulani ni binadamu hakuna wa
kuiondoa. Ni haki anayoitoa mungu tu.
Ni
haki ya kuzaliwa ambayo mtu hawezi kupewa na mtu mwingine. Ni haki ambayo
huwezi kuifananisha na haki nyingine yoyote. Ina thamani kubwa na kuiondoa au
kujaribu kuifubaza au kuiua kwa kumweka mtu sehemu zenye mikojo na wadudu ni
kinyume kabisa cha uungwana.Si kumdhalilisha yule pekee isipokuwa ni kuudhalilisha
ubinadamu kwa ujumla wake akiwemo yeye
anayetekeleza ubaya huo.
0784482959
0714047241
0 comments:
Post a Comment